Dar es Salaam. Dhamira ya Tanzania kujenga uchumi usio tegemea sana fedha taslimu imepata msukumo mpya baada ya kampuni ya kimataifa ya Visa, kuzindua rasmi ofisi yake nchini Tanzania.
Tukio kuu, lililojulikana kama Visa Day, liliwaleta pamoja wadau muhimu, maofisa wa serikali, wasimamizi wa sekta na viongozi wa tasnia chini ya paa moja jana jijini Dar es Salaam.
Upanuzi wa Visa katika soko la Tanzania unajumuisha uteuzi wa Meneja Mkazi Victor Makere, ambaye atasimamia shughuli za Visa nchini Tanzania, Uganda, Burundi na Rwanda.
Hatua hii inaonesha dhamira ya muda mrefu ya Visa kwa uchumi wa kidijitali unaokua kwa kasi ukanda wa Afrika Mashariki huku wakiahidi kushirikiana moja kwa moja na wafanyabiashara na watumiaji wa ndani.
“Visa imekuja karibu zaidi na wateja wake hapa Tanzania ili kuwezesha mifumo ya malipo iliyo rahisi, salama na yenye ufanisi,” alisema Makere wakati wa uzinduzi huo.
Aliongeza kuwa Visa inalenga kujikita kwa kina katika sekta mbalimbali za uchumi ikiwamo utalii, teknolojia na ubunifu, elimu, kilimo na nyingine kwani suluhu za malipo kidijitali zinaweza kuleta mabadiliko makubwa.
“Hatujaja tu kutoa huduma; tunataka kujipenyeza katika mfumo wa uchumi wa nchi,” alisema Makere na kuongeza kuwa Visa itasaidia kuunganisha wafanyabiashara na watumiaji wa Tanzania na sekta kuu za uchumi katika nchi nyingine.
Ili kuwahakikishia watumiaji usalama, Makere alieleza kuwa mifumo ya Visa imejengwa kwa teknolojia ya juu, imara na inayoheshimika duniani kote sanjari na ulinzi wa taarifa binafsi na za kifedha.
“Visa inafanya kazi kwa viwango vya juu kabisa vya kimataifa vya usalama wa mitandao na faragha ya data. Watu hawapaswi kuwa na wasiwasi kuhusu usalama wa taarifa zao tumejikita kudumisha imani yao katika kila hatua ya safari ya malipo ya kidijitali.”
Katika hotuba yake wakati wa uzinduzi huo Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Emmanuel Tutuba, alielezea kuwa hiyo ni hatua muhimu inayodhihirisha imani ya kimataifa katika uchumi wa Tanzania na mafanikio ya mageuzi ya ndani katika kusaidia ubunifu wa kidijitali.
“Kuanzisha ofisi yako hapa Tanzania kunamaanisha unapata fursa ya soko lote la takribani watu bilioni 1.4 barani Afrika,” aliongeza, akitaja ushiriki wa Tanzania katika Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), SADC na Eneo Huru la Biashara la Bara la Afrika (AfCFTA).
Tutuba alibainisha kuwa kufikia Mei 2025, mzunguko wa fedha za kielektroniki ulikuwa umefikia zaidi ya Sh2.18 trilioni, huku kukiwa na zaidi ya laini za simu milioni 66 zenye usajili hai nchini, takwimu zinazothibitisha mwelekeo wa nchi kuelekea mfumo wa fedha wa kidijitali.
“Malipo ya kidijitali sasa siyo tena shughuli ya anasa kwa wachache, kwa sababu inaonekana kwa sasa ni kama hitaji muhimu kwa Watanzania,” alisema.
Naye Kiongozi wa Visa kwa Kanda ya Kusini na Mashariki mwa Afrika, Michael Berner, alisisitiza tena dhamira ya kampuni hiyo kuchangia mageuzi ya kiuchumi ya Tanzania.
“Wajasiriamali wadogo na wa kati (SMEs) ndio uti wa mgongo wa uchumi karibu kila sehemu duniani, na Tanzania pia siyo tofauti,” alisema Berner huku akieleza kuwa uchunguzi wao unaonesha kuwa asilimia 84 ya SMEs nchini Tanzania tayari wameanza kutumia malipo ya kidijitali katika biashara zao.
Aidha alisema Visa inapanga kuanzisha huduma kama ‘Visa Direct’ kwa ajili ya malipo ya papo kwa papo kuvuka mipaka, ujumuishaji na pochi za kielektroniki (mobile wallets), malipo bila kugusa kadi na yale yaliyofichwa kwa teknolojia ya tokeni.