WAKATI ikielezwa klabu ya Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini ikirudi Azam FC ikiwa na dau ya Dola 350,000 ili kumnasa kiungo mshambuliaji wa timu hiyo, Feisal Salum ‘Fei Toto’, huku tetesi zingine zikisema kuwa yupo mbioni kurejea Yanga, mabosi wa matajiri hao wameibuka na kutoa msimamo.
Mabosi wa klabu hiyo iliyomaliza katika nafasi ya tatu katika Ligi Kuu Bara iliyomalizika mwezi uliopita, wamesisitiza kuwa, bado kwa sasa Fei Toto hauzwi kwani hajamalizana nao na wala hakuna mazungumzo yoyote rasmi juu ya kuhitajiwa na Yanga kwa nyota huyo wa zamani wa JKU.
Mkuu wa Idara ya Mawasiliano na Habari wa Azam, Thabit Zakaria ‘Zakazi’ amesema kiungo huyo bado hajamalizana na klabu yake na hakuna mazungumzo yoyote.
Fei aliyewahi kukipiga JKU, alitamba na Yanga kabla ya kumtimkia Azam ambako alisaini mkataba wa miaka mitatu na unatarajiwa kumalizika msimu ujao.
Akizungumza na Mwanaspoti, Zakazi alisema hadi sasa kinachoendelea kuhusu Fei Toto ni tetesi tu za mitandaoni ila ukweli ni kwamba hata hizo timu hazijafanya mazungumzo yoyote na Azam.
“Fei ni mchezaji wetu na bado ana mkataba na hatuna mpango wa kumuuza hata hao wanaomtaka wanajua kwamba hilo haliwezekani ndio maana hawajafanya mazungumzo na sisi,” alisema Zakazi na kuongeza;
“Tha-mani anayoipata Fei sasa hivi imekuja baada ya kutua Azam, kwani alivyokuwa timu zingine si walikuwa wanamuona mbona hawakumtamani au kumnunua? Azam imeongeza thamani ya Fei kwa kumpa nafasi ya kuwa staa anayewaongoza wenzake uwanjani kutengeneza ushindi, lakini zaidi makocha wamemjenga kiufundi ndio maana ameweka rekodi ambazo hajawahi kuweka alikokuwepo.”
Zakazi alikiri uwepo wa Fei umekuwa msingi mzuri hasa kwa wale watoto wanaocheza katika timu yao ya vijana, kwani amekuwa akipata muda wa kucheza nao na kuwafundisha.
“Pesa tuliyotoa kumnunua Fei imerudi mara mbili, kwani ujio wake uliongeza mashabiki wengi kwa upande wetu ambao hadi sasa wamekuwa wateja wa jezi zetu,” alisema Zakazi na kuongeza;
“Hivyo kuwa na mchezaji tena mzawa ambaye anawatikisa hata wageni kwetu ni faraja na yeye anafahamu jinsi tunavyomthamini na kuheshimu kile anachokifanya, ni mchezaji mzuri kiukweli.”
Mwanaspoti iliwahi kuandika tetesi kuwa mabosi wa Simba na Yanga wanammezea mate kiungo huyo licha ya kuwa hajamaliza mkataba, ila hakuna kati yao aliyewafuata mabosi zake ili kumnunua.
Rekodi zake ndani ya misimu miwili zimekuwa za moto kwani mwaka wake wa kwanza Azam alimaliza na mabao 19 akikimbizana na MVP Stephane Aziz KI aliyefunga mabao 21 na msimu huu amemaliza na mabao manne na kuwa kinara wa asisti akiwa na 13.