Kisa ‘Tshabalala’ Simba, Yanga zaingia vitani wamo pia Waarabu

BEKI wa kushoto wa Simba, Mohamed Hussein ‘Tshabalala’ amezidi kuwapasua vichwa mabosi wa klabu hiyo na wale wa mtaa wa pili kutoka Yanga, ambao wameingia vitani kunasa saini yake, huku Waarabu wakiendelea kufanya mazungumzo naye.

Tshabalala aliyeitumikia Simba kwa zaidi ya miaka 10 tangu 2014 ilipomsajili akitokea Kagera Sugar na kupita mikononi mwa makocha 16 mkataba wake na Wekundu hao umemalizika kwa sasa na mabosi wa Simba wamedaiwa kuanza mazungumzo naye, huku Yanga nao wakipambana kuinasa saini yake.

Baada ya Tshabalala kumaliza mkataba na Simba msimu uliomalizika, hakufanya makubaliano na mabosi hao ili kuongeza kandarasi kama ilivyokuwa katika miaka ya nyuma.

Msimu ulipomalizika tu mabosi hao walimuita na kukaa naye chini ili kujadiliana kuhusu mkataba mpya lakini beki huyo aliomba kupewa muda zaidi.

Taarifa za ndani zimelidokeza Mwanaspoti kuwa; “Tshabalala bado anasikilizia ofa alizopewa na mabosi hao licha ya kwamba hazijawekwa wazi ila hicho ndicho kinachoendelea kwani mabosi wa wekundu wanajua kabisa kuwa hawana mbadala wake.”

Wakati mabosi wa Simba wakisubiri majibu ya mkongwe huyo, Yanga na timu moja ya Uarabuni nazo ziko mlangoni zikimuhitaji beki huyo kwa ajili ya msimu ujao.

Taarifa za ndani zinasema; “Yanga inahitaji beki wa kushoto mzawa ambaye atakwenda kusaidiana na Chadrack Boka, kwani mabosi hao wanataka kumrudisha Nickson Kibabage Singida Black Star.

“Timu nyingine ni Bahrain Sport Club iliyoko Uarabuni, hivyo uongozi wa beki huyo bado unachekecha ofa ipi ya kwenda nayo.”

Ikumbukwe kuwa, hii sio mara ya kwanza kwa Yanga kumuwania beki huyo kwani tetesi ziliwahi kusikika miaka ya nyuma kwamba Yanga inamfukuzia bila mafanikio.

Tshabalala aliwahi kuzungumza na Mwanaspoti na kuliambia kuwa, siri ya kusalia katika ubora mzuri kwa kipindi kirefu ni kwa sababu aliamua kuzingatia kila kitu alichofundishwa na makocha na pia kutoendekeza starehe.

“Mimi ni mtu wa familia sana kama nisipokuwa kambini basi niko nyumbani na familia, lakini nazingatia sana vyakula sili kila kitu ila msosi wangu ni ule unaojenga mwili tu, sinywi pombe au vinywaji vyenye sukari nyingi.

“Bado nina ndoto za kwenda nje ya nchi kucheza soka kwa sababu kuna faida yake hasa kuitangaza nchi na kuongeza uzoefu na timu zimewahi kunifuata lakini hatukuafikiana.

“Ofa za timu zilizokuja sikuridhika nazo ndio maana sikwenda kucheza nje ila ikija nzuri kwa nini nisiende kuongeza uzoefu na kukutana na changamoto mpya.” 

Akiwa na jezi ya Simba Tshabalala ametwaa mataji mengi ikiwamo ubingwa wa Ligi Kuu Bara mara nne, Ngao ya Jamii mara tano, Kombe la Muungano mara moja.

Pia ameiwezesha Simba kufanya vizuri kwenye michuano ya CAF akiifikisha robo fainali ya Ligi ya Mabingwa mara nne na Fainali ya Kombe la Shirikisho mara moja.

Bila kusahau umuhimu wake katika kikosi cha timu ya Taifa Stars ambapo amecheza fainali za mataifa ya Afcon mara mbili kati ya tatu ambazo Stars imeshiriki.