Too Much wababe mashindano ya Ngalawa

NGALAWA ya Too Much imeibuka mshindi wa kwanza katika mbio za ngalawa, kati ya tisa zilizoshiriki mashindano hayo yaliyofanyika Fumba, Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja.

Katika mashindano hayo, nafasi ya pili imekwenda kwa Wape Kazi, huku Ubaya Ubwela ikishika nafasi ya tatu. Utoto Raha imeshika nafasi ya nne, Atoae Mola (5), Mungu Ibariki (6), Msihofu (7), Safiria Nyota Yako (8), na Sio Wote (9). 

Mashindano hayo ni sehemu ya kurudisha michezo ya asili visiwani hapa kuwa utambulisho wa kiutamaduni ambapo imeonekana kuwa bado michezo hiyo ina nafasi katika kujenga jamii yenye umoja na mshikamano.

Akizungumza baada ya ushindi huo, Nahodha wa Too Much, Mahmoud Abdalla Juma amesema kuwa siri ya mafanikio hayo ni kumtegemea Mungu pamoja na uimara wa chombo chao kinachohimili mawimbi makali ya baharini.

“Mungu ndiye muongozaji wetu bila ya yeye tusingefanikiwa na tunashukuru mashindano haya ya kipekee ambayo yanatufanya tujisikie kuwa sehemu ya jamii yetu,” amesema Mahmoud.

Naye mratibu wa mashindano hayo, Mohammed Abdalla Mohammed, amesema mashindano hayo yamerudishwa rasmi mwaka 2013 baada ya kusimama kwa muda mrefu ikiwa lengo ni kuwaunganisha wananchi wa vijiji jirani kupitia mchezo huo.

Amesema pamoja na changamoto za kiutendaji, msaada wa kisheria kutoka kwa Legal Services Facility (LSF) na Idara ya Katiba na Msaada wa Kisheria umesaidia kufanikisha mashindano hayo kwa mafanikio makubwa.

“Tunataka michezo ya asili kama hii idumu na kurithishwa kwa vizazi vijavyo. Ni urithi wa utamaduni wetu,” amesema Mohammed. 

Naye Mkuu wa Wilaya ya Magharibi B, Amour Yussuf Mmanga, amesema michezo ina mchango katika kudumisha mshikamano na kueleza kuwa mashindano hayo ni daraja la kujenga umoja, urafiki na historia miongoni mwa wanajamii.