Dodoma. Baada ya ukimya wa muda mrefu, hatimaye Mwenyekiti wa zamani wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe ameibukia kwenye uzinduzi wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025-2050.
Uzinduzi huo unafanyika leo Alhamisi, Julai 17, 2025 katika Ukumbi wa Jakaya Kikwete jijini Dodoma, ambapo wageni mbalimbali wamehudhuria na mgeni rasmi ni Rais Samia Suluhu Hassan ambaye amefika ukumbini.
Tangu aliposhindwa kutetea kiti chake cha uenyekiti ndani ya Chadema dhidi ya Tundu Lissu, Mbowe amekuwa haonekani mara kwa mara hadharani. Hivi karibuni ameonekana shughuli za kanisani na misibani.
Uchaguzi mkuu wa Chadema uliohitimisha uongozi wa miaka 21 wa Mbowe ndani ya chama hicho, uliofanyika Januari 21, 2025 katika Ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam na matokeo kutangazwa kesho yake ya Januari 22.
Mbowe alikubali matokeo na kueleza anakwenda kujikita zaidi kwenye shughuli za kibiashara ambazo alidai alikosa muda wa kutupia macho huko kutokana na muda mwingine kuuelekeza kwenye siasa.
Hata hivyo, kwa mujibu wa katiba ya Chadema, Mbowe anaendelea kuwa mjumbe wa kudumu wa kamati kuu ya chama hicho na tangu Januari hadi sasa, hajawahi kushiriki Kikao chochote cha kamati kuu.
Leo Alhamisi Julai 17,2025, Mbowe ameonekana akiingia ukumbi kushiriki uzinduzi wa Dira hiyo 2050.
Mbowe amekaa mstari wa mbele katika ukumbi huo pamoja na viongozi mbalimbali wa kisiasa, wafanyabiashara, wawekezaji na mawaziri.
Endelea kufuatilia Mwananchi