Dar es Salaam. Wakati dunia ikishuhudia maendeleo ya kasi katika biashara za ndani na za kuvuka mipaka, bara la Afrika linaendelea kupambana na changamoto nyingi zinazokwamisha ndoto yake ya kuwa kitovu cha biashara na ukuaji wa uchumi wa dunia.
Ingawa Afrika inajivunia rasilimali nyingi za asili na idadi kubwa ya watu, wachambuzi wa uchumi wanasema kinachokosekana ni mtazamo wa pamoja wa uwekezaji, miundombinu bora, na mifumo rafiki kwa ujasiriamali.
Wakati wa Kongamano la Biashara Barani Afrika (Unlocked Africa) lililoandaliwa na Benki ya Standard Group, lililofanyika Cape Town, Afrika Kusini, Ofisa Mtendaji Mkuu wa kampuni ya Simba Group David Ndelwa alielezea namna ambavyo changamoto za miundombinu ya usafirishaji na mifumo ya malipo zinavyokwamisha biashara kwa wengi.
“Afrika tuna soko huru (AfCTA) lakini linakosa ufanisi kwa sababu ya hizo changamoto. Hii ni tofauti na hali iliyopo katika bara la Ulaya kupitia EU wao wanapotaka tija zaidi kwa sababu ya urahisi ya kufanya biashara walionao miongoni mwao,” anasema Ndelwa.
Anasema miundombinu ya usafiri katika Bara la Afrika inakwamisha kushamiri kwa biashara ya ndani lakini pia gharama kubwa za usafiri wa anga zinaleta ugumu kwa wajasiriamali kutoka eneo moja kwenda lingine.
“Mimi nafanya biashara kwenye nchi 7 Afrika, mfano mdogo tu hamna barabara ya moja kwa moja kwenda Maputo kutokea Dar es Salaam. Katika nchi nyingine ili kwenda unahitaji visa lakini jumuiya zilizofanikiwa kama Umoja wa Ulaya (EU) usafiri wa watu na vitu umerahisishwa,” anasema.
Ndelwa anasema changamoto nyingi ni mifumo ya malipo isiyosomana kwa mataifa zaidi ya 50 kila moja lina sarafu yake na lina mfumo wake wa fedha hivyo kufanya malipo miongoni mwa wananchi inakuwa shida.
“Mfumo wa malipo wa pamoja utaleta suluhu kubwa ya biashara kwani ilivyo sasa kila nchi ili kufanya biashara nchini sarafu inayotumika ni Dola ya Marekani jambo ambalo linaongeza ugumu katika biashara,” anasema Ndelwa.
Hata hivyo Ndelwa anasema Afrika ina fursa kubwa ya kubadili mtazamo wake wa kiuchumi kwa kuboresha maeneo yenye changamoto lakini zaidi eneo la malipo.
Anasema maeneo mengine yanayoweza kuleta ufanisi wa biashara ndani ya bara hili ni kuboresha mazingira ya kisasa na kukuza ujuzi miongoni mwa watu wake ili kuutumia ujuzi huo kuongeza uzalishaji mali.
Katika kongamano hilo Mkurugenzi Mtendaji wa benki hiyo, Sim Tshabalala alisema serikali za Afrika zinapaswa kutunga sera za ndani zitakazopunguza urasimu na kuwezesha upatikanaji rahisi wa mikopo.
“Mustakabali wa Afrika haupo kwenye misaada ya huruma, bali uko kwenye ubunifu, ustahimilivu, na biashara. Tukipata nyenzo sahihi, SMEs zetu zinaweza kuwa injini ya ustawi wa pamoja.”
Tshabalala anasema kwa kutorasimisha biashara ndogo zisizo rasmi, wajasiriamali wa bara hili wataendelea kukosa mitaji.
Naye Mkuu wa utafiti wa Benki ya Standard Group, Goolam Ballim anasema changamoto ya mifumo ya malipo ndani ya bara la Afrika itatatuliwa na maendeleo ya ubunifu katika huduma za kifedha (Fintech).
Anasema suala la mifumo ya malipo limekuwa likibadilika kwa miaka mingi na Afrika inajijengea mfumo wake mpya ambao utakuwa na matokeo makubwa ambao ni huduma za miamala ya simu ambazo zimeenea maeneo mengi ya bara hili.
“Hitaji kubwa la Bara la Afrika ni kuunganishwa katika shughuli zake na uzuri ni bara lenye rasilimali nyingi ikiwamo rasilimali watu,” anasema Ballim.
Namna ya kukuza ujasiriamali
Akizungumza katika kongamano la biashara lililoandaliwa na Benki ya Standard Group, Makamu wa Rais wa Botswana Ndaba Gaolathe anasema ili kubadilisha hali iliyopo ni lazima mataifa ya Afrika yabadili mtazamo wake na kukumbatia zaidi ujasiriamali.
Kiongozi huyo ambaye alikuwa mgeni rasmi katika siku ya kwanza ya kongamano hilo lililokutanisha magwiji wa biashara barani Afrika amesema bara hili lina hazina kubwa ya fursa ambazo hazijachangamkiwa hivyo kinachotakiwa ni mabadiliko ya kubadili hali.
“Makadirio yanaonyesha kuwa ifikapo mwaka 2050 idadi ya watu Afrika itakuwa Bilioni 2.5 na hivi sasa kati ya watu zaidi ya bilioni 1.5 waliopo asilimia 60 ni vijana tena sio vijana tu bali wenye uwezo thabiti lakini kiwango cha mitaji binafsi kinachovutiwa barani Afrika ni asilimia moja ya kiwango chote cha ulimwengu. Tunapaswa kubadili hili,” amesema.
Alisema bara la Afrika halihitaji kusaidiwa bali linahitaji miundombinu, mitaji na utekelezaji wa mipango endelevu. “Tufikirie fursa zilizopo bara la Afrika kwa ukubwa wake, tusiwaze mabilioni tuwaze matrilioni na sekta binafsi ina nafasi ya kutufikisha kwenye mafanikio”.
Kuhusu fursa za mkutano huo Mkurugenzi wa kampuni ya Ona Safari, Julias Mkondo anasema kongamano hilo ni jukwaa muhimu kwake kupata uzoefu wa namna wenzake katika bara la Afrika wanaendesha na kusimamia biashara.
“Changamoto kubwa kwa tulio wengi (wajasiriamali) mitaji. Tukiweza kupata mitaji kwa urahisi tutakuza biashara zetu na kutimiza malengo ya kuongeza mchango wa sekta tuliyopo,” amesema Mkondo ambaye kampuni yake inahusika na huduma za utalii nchini Tanzania.
Anatolea mfano Tanzania ambako Serikali ina malengo ya kuvutia watalii milioni tano akisema taasisi za fedha zinapaswa kuangalia mahitaji ya watoa huduma katika sekta hiyo akisisitiza kuwa eneo la malazi lina fursa kubwa lakini kinachokwamisha ni mitaji.
Hata hivyo Mkuu wa Idara ya Biashara wa Benki ya Stanibic Tanzania ambayo ni benki tanzu ya Benki ya Standard, Charles Mishetto yeye anasema kuwa Tanzania kinachofanywa na benki hiyo ni kurasimisha shughuli za ujasiriamali ili iwe rahisi kuzipatia mitaji.
“Benki nyingi zinakopesha kwa kuangalia dhamana kwetu sisi dhamana ni miamala yako lakini lazima tukuwezeshe kuwa rasmi ili kukidhi mahitaji ya kibenki,” amesema Mishetto hukua akisisitiza kuwa wanafanya urasimishaji kupitia kampeni zao mbalimbali.