Watu wengi na hasa wasomaji wa gazeti hili wamekuwa na uelewa wa mambo kadhaa yanayohusu fedha na uwekezaji.
Makala iliyopita iliangazia ni namna gani unavyoweza kukadiria kiasi cha akiba. Kama vile mkulima anavyoweza kukadiria kiasi cha ardhi alime ili apate mavuno anayotarajia kwa msimu wa kilimo, swali la msingi kwenye uwekezaji ni kuwa ni uwekeze kiasi gani ili uweze kupata faida yenye tija.
Uwekezaji ni moja ya njia muhimu za kujenga utajiri na kutoa usalama wa kifedha kwa siku zijazo. Hata hivyo, kiwango cha uwekezaji ambacho mtu wa kawaida anaweza kufikia kinategemea sana mazingira ya kiuchumi, kijamii na sehemu unayoishi kama ni mjini au kijijini.
Mtu wa kawaida hapa anamaanisha mwananchi wa wastani, kama mfanyakazi wa kawaida, mfanyabiashara mdogo au mkulima, ambaye mapato yake yanategemea mishahara ya chini au mazao ya kilimo.
Kama nchi nyingine zote, uwekezaji unategemea kiwango cha mfumuko wa bei, hali ya umasikini na pia uwezo mdogo wa matumizi.
Pia kama nchi, tunao utegemezi mkubwa wa bidhaa za viwandani na mitambo ya uzalishaji kutoka nje ya nchi. Uwekezaji unalipa kukiwa na mazingira mazuri ya ufanyaji wa biashara hasa kutumia rasilimali za ndani.
Kama tulivyoona kwenye makala zilizopita, ni vizuri kuwaza uwekezaji baada ya kuweka akiba inayotosheleza, kama akiba ya dharura inayoweza kugharamia gharama za maisha kwa angalau miezi mitatu hadi sita. Hii ni muhimu kwani uwekezaji ni jambo la muda mrefu na haupaswi kuathiri sehemu au uwekezaji wako wote kwa kutumia kwenye matumizi ya kawaida.
Kama vile mkulima wa mazao ya nafaka anavyofikiria alime kiasi gani cha ardhi kutokana na zana na uwezo wake pia kama anataka kutosheleza familia yake kwa chakula au apate na ziada ya kuuza, hivyo hivyo na mwekezaji anavyopaswa kufikiri.
Mkulima anavyoandaa shamba anakuwa amejiwekea akiba ya chakula kuanzia matayarisho ya shamba hadi anapovuna. Hivyo ni vizuri kufikiria kuwa na fedha za akiba tofauti na zile za uwekezaji.
Kiwango cha uwekezaji kwa mtu wa kawaida kinategemea moja kwa moja mapato yake. Kwa ulinganifu wa urejeshwaji katika uwekezaji unatakiwa kukulipa rejesho la mwaka ambalo ni kubwa kuliko riba inayotolewa na benki ama taasisi nyingine za kifedha. Hii ni kwa sababu benki inavyokukopesha kufanya biashara inategemewa upate faida ya kutosha kurudisha gharama ya mkopo na kufanya matumizi mengine.
Ni vizuri kuangalia tahadhari na kiwango cha urejeshwaji. Ukiwekeza unaweza kupata rejesho ama fedha ulizowekeza zikapotea kiasi ama zote. Ili kuweza kupata tija kwenye uwekezaji ni muhimu kuwekeza kwenye maeneo mbalimbali.
Urejeshwaji wenye tija ni pale ambapo utapata mavuno yanayoweza angalau kulipia gharama zako kila mwezi kwa uwekezaji uliofanya na kuweka akiba uliyojipangia kwa mwezi.
Ni muhimu kutambua kuwa uwekezaji sio ajira. Unaweza kuwa umewekeza huku una ajira yako. Unaweza pia ukawa unawekeza kama njia ya kujipatia ajira hivyo uwekezaji huo unapaswa kukulipa mapato ambayo yanakidhi mahitaji yako ya mwezi na kuweka akiba, huku ukilinda mtaji kwenye uwekezaji.
Kama uwekezaji unaoufanya haujaleta tija inayohitajika endelea kuwekeza na badili njia na mbinu za uwekezaji. Uwekezaji kama ilivyo kwa uwekaji wa akiba ni tabia ambayo inapaswa kuwa endelevu. Kama ambavyo mkulima wa kawaida analima au kufuga kila siku na kila mwaka ndivyo inapaswa kuwa kwa mwekezaji makini.