Aucho aigomea Yanga, kuibukia huku!

HAKUNA ubishi mashabiki wa Yanga wanafahamu kuna baadhi ya mashine zilizowapa heshima msimu uliopita kwa kutwaa mataji matano zinaweza kuondoka kwa ajili ya kusukwa upya kwa kikosi kijacho kwa msimu mpya wa mashindano.

Hata hivyo, hakuna aliyeliweka akilini jina la Khalid Aucho kutokana na nyota huyo raia wa Uganda kuwa kipenzi cha Wanajangwani na hasa walipohakikishiwa na mabosi wao, kwamba wapo katika mazungumzo ya kumpa mkataba mpya wa kuitumikia timu hiyo.

Lakini kitu cha kushtua ni kwamba kiungo huyo maarufu kama ‘Daktari wa Mpira’ kwa sasa anahesabu saa tu kabla ya kutimka baada ya kugomea ofa aliyopewa na mabosi wa klabu hiyo, huku nyota na straika wa zamani wa timu hiyo, Kennedy Musonda aliyeaga hivi karibu na kutua Israel akitajwa.

Aucho ambaye Yanga ilimtambulisha rasmi Agosti 9, 2021 kuwa kiungo wao mpya akitokea Misri, amekuwa sehemu kubwa ya mafanikio ya ubingwa na makali ya kikosi cha timu hiyo.

Taarifa za uhakika ambazo Mwanaspoti imezipata ni kwamba, awali kiungo huyo raia wa Uganda alikuwa ameshakubaliana kila kitu na uongozi wa Yanga kwamba atasaini mkataba wa mwaka mmoja kusalia ndani ya timu hiyo.

Hata hivyo, mambo yamebadilika fasta, baada ya kushindwa kukubaliana juu ya dau la usajili kubadilika kutoka upande wa kiungo huyo.

Mabadiliko hayo yalitokana na ofa mbili ambazo kiungo huyo amezipokea ndani ya wiki chache tangu arudi kwao Uganda kwa mapumziko.

Ingawa Aucho ameshindwa kujibu taarifa hizo, lakini Mwanaspoti linafahamu kwamba, kiungo huyo alipewa ofa ya Dola 45,000 kwenda Israel ikielezwa amefanyiwa mchongo na swahiba wake, Musonda huku pia akiwa na ofa ya Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini inayompigia hesabu.

Inadaiwa kuwa, Aucho alitaka Yanga impe Dola 35,000-40,000 ili aweze kubaki hatua ambayo iliwalazimu mabosi wa klabu hiyo kuomba muda wafikirie zaidi.

Yanga wasiwasi wao ulikuwa ni gharama hizo kubwa, lakini namna kiungo huyo alivyotumika msimu uliopita, akikosa baadhi ya mechi nyingi kutokana na majeraha.

Msimu uliopita Aucho alicheza mechi 22, akitumia dakika 1735 uwanjani, akifunga bao moja dhidi ya Mashujaa kwenye ushindi mkubwa wa mabao 5-0 na kutoa asisti moja.

Mabosi wa klabu hiyo wakaenda mbali zaidi wakiona hata hatua ya wao kuingia sokoni kutafuta kiungo mkabaji wa shoka kama Moussa Bala Conte wanayeipigania saini yake ni kutokana na wasiwasi wa kumpoteza Aucho.

“Unapofanya uamuzi mkubwa lazima uangalie ni nani unampa fedha kama hizo, sote tunafahamu kwamba Aucho kama yuko sawa ni kiungo wa kazi hasa, lakini kwasasa uhakika huo ni vigumu kuupata ukiangalia tu msimu uliomalizika,” alisema bosi huyo wa juu na kuongeza;

“Kwa hiyo uwezekano wa kubaki ni mdogo sana, ni ngumu kukubali kumuachia lakini kuna wakati unalazimika kukabiliana na changamoto mpya, tutapata watu wengine bora.”

Inadaiwa Aucho alikerwa na hatua ya Yanga kuwa kimya baada ya kuomba muda wa kutafakari ofa ambayo aliwapa kupitia mazungumzo ya mwisho.

Mwanaspoti linafahamu kwamba kufuatia ukimya huo wa mabosi wa Yanga, Aucho ameamua kusaka maisha mapya baada ya mkataba wake kumalizika mwisho wa msimu uliopita.