Senegal kuziba nafasi ya Congo Brazzaville mashindano ya CECAFA

Timu ya Taifa ya Senegal itashiriki Mashindano maalum ya CECAFA yatakayo husisha mataifa manne kabla ya mashindano ya CHAN yanayotarajiwa kuchezwa Julai 21-27, 2025 kwenye Uwanja wa Black Rhino, Karatu jijini Arusha.

Senegal inachukua nafasi ya Congo Brazaville ambayo imekumbana na changamoto na kushindwa kufanya safari kama ilivyokuwa imepangwa awali.

Hayo yameelezwa na Mkurugenzi Mtendaji wa CECAFA, Auka Gecheo katika taarifa yake aliyotoa kwa vyombo vya habari leo Julai 17, 2025.

“Tunafuraha kutangaza kwamba Senegal imekubali kushiriki Mashindano hayo baada ya Congo Brazzaville kueleza kuwa wamekumbana na changamoto za vifaa na hawakuweza kufanya safari kama ilivyopangwa awali”.

Shirikisho la Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) limeamua kuandaa michuano hiyo ili kuzipa nafasi timu za ukanda huu kujiandaa na michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wa ndani (CHAN) 2024.  mwezi Agosti.

Kwa sasa Taifa Stars ipo Misri ikiendelea na kambi iliyoanza Julai 7 mwaka huu jijini Dar es Salaam ikijiandaa na michuano ya CHAN itakayofanyika Tanzania kwa kushirikianma na Kenya na Uganda kuanzia Agosti 2 hadi 30, mwaka huu.

Michuano ya CHAN itashirikisha timu za taifa kutoka nchi 19, ambapo Kundi A mechi zake zitachezwa kwenye Uwanja wa Kasarani nchini Kenya, zikishirikisha Kenya, Morocco, Angola, DR Congo na Zambia, huku kundi B zikichezwa Dar es Salaam, zikiundwa na Tanzania, Madagascar, Mauritania, Burkina Faso na Jamhuri ya Afrika ya Kati.

Mechi za kundi C ambazo zitachezwa Uganda, zitashirikisha Uganda, Niger, Guinea, Afrika Kusini na Algeria, huku kundi D ambalo mechi zake zitapigwa kwenye Uwanja wa Amaan Complex visiwani Zanzibar, litashirikisha Senegal, Congo, Sudan na Nigeria.

Julai 21, 2025, Uwanja wa Black Rhino.
– Kenya vs Uganda

Julai 22, 2025, Uwanja wa Black Rhino.
– Tanzania vs Senegal

Julai 24, 2025, Uwanja wa Black Rhino.
– Senegal vs Uganda.
– Tanzania vs Kenya.

Julai 27, 2025, Uwanja wa Black Rhino.
– Kenya vs Senegal
– Uganda vs Tanzania.