Simba yatozwa faini ya jumla Sh3 milioni kwa kutofuata kanuni za Ligi

Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi ya Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) katika kikao chake cha Julai 15, 2025 ilipitia mwenendo na matukio mbalimbali ya Ligi na kuitoza Simba faini ya jumla ya Sh3 milioni katika makosa matatu waliyoyafanya timu hiyo katika mchezo namba 184 dhidi ya Yanga.

Klabu ya Simba imeadhibiwa kwa kutozwa faini ya Sh1 milioni kwa kosa la kushindwa kuhudhuria mkutano wa wanahabari ulifanyika kwenye ukumbi wa Benki ya Taifa ya Biashara, Dar es Salaam Juni 24, 2025 kinyume na matakwa ya Kanuni ya 17:58 ya Ligi Kuu kuhusu Taratibu za Mchezo.

Adhabu hii ni kwa mujibu wa kanuni ya 17:62 ya Ligi Kuu kuhusu Taratibu za Mchezo.

Katika hatua nyingine Simba imeadhibiwa kwa kutozwa faini ya Sh1 milioni kwa kosa la kushindwa kuhudhuria kikao cha kitaalam cha maandalizi ya mchezo (MCM) Juni 24, 2025 kinyume na matakwa ya Kanuni ya 17:2(2.2) ya Ligi Kuu kuhusu Taratibu za Mchezo.

Adhabu hii ni kwa mujibu wa kanuni ya 17:62 ya Ligi Kuu kuhusu Taratibu za Mchezo.

Aidha Klabu ya Simba imeadhibiwa kwa kutozwa faini ya Sh 1 milioni kwa kosa la kuingia kwenye uwanja wa Benjamin Mkapa kupitia mlango usio rasmi kuelekea mchezo huo uliochezwa Juni 25, 2025, kinyume na matakwa ya kanuni ya 17:21 ya Ligi Kuu kuhusu Taratibu za Mchezo.

Adhabu hii ni kwa mujibu wa kanuni ya 17:62 ya Ligi Kuu kuhusu Taratibu za Mchezo.

Adhabu zingine zilizotolewa na kamati ni kama ifuatavyo

MECHI NAMBA 229: KENGOLD FC 0-5 SIMBA SC

Timu ya KenGold ya mkoani Mbeya imepewa Onyo Kali kwa kosa la kuchelewa kuingia kwenye uwanja wa Ali Hassan Mwinyi, Tabora kuelekea mchezo tajwa hapo juu Juni 18, 2025.

KenGold iliingia uwanjani saa 9:35 alasiri badala ya saa 8:30 mchana jambo ambalo ni kinyume na matakwa ya Kanuni ya 17:15 ya Ligi Kuu kuhusu Taratibu za Mchezo.

Adhabu hii ni kwa mujibu wa Kanuni ya 17:62 ya Ligi Kuu kuhusu Taratibu za Mchezo.

MECHI NAMBA 231: AZAM FC 5-0 TABORA UNITED FC

Klabu ya Tabora United imetozwa faini ya Sh. 1,000,000 (milioni moja) kwa kosa la kushindwa kuhudhuria mkutano wa wanahabari kwenye ukumbi wa Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) Dar es Salaam Juni 17, 2025 kinyume na matakwa ya Kanuni ya 17:58 ya Ligi Kuu kuhusu Taratibu za Mchezo.

Adhabu hii ni kwa mujibu wa kanuni ya 17:62 ya Ligi Kuu kuhusu Taratibu za Mchezo.

MICHEZO YA MTOANO (PLAY-OFF) HADHI YA LIGI KUU BARA

MECHI NAMBA PO1: STAND UNITED 1-3 FOUNTAIN GATE

Klabu ya Fountain Gate imetozwa faini ya Sh. 1,000,000 (milioni moja) kwa kosa la kikosi chake kulazimisha kupita katika eneo lililotengwa na kuwekewa uzio kwa ajili ya shughuli ya uzalishaji maudhui ya mchezo huo inayofanywa na mdhamini mwenye haki za matangazo ya runinga, Azam Media Limited.

Adhabu hii ni kwa mujibu wa kanuni ya 17:62 ya Ligi Kuu kuhusu Taratibu za Mchezo.

Klabu ya Fountain Gate imetozwa faini ya Sh. 1,000,000 (milioni moja) kwa kosa la kukataa kutumia chumba maalum cha kuvalia kwenye uwanja wa Kambarage, Shinyanga kinyume na matakwa ya Kanuni ya 17:20 ya Ligi Kuu kuhusu Taratibu za Mchezo.

Adhabu hii ni kwa mujibu wa kanuni ya 17:62 ya Ligi Kuu kuhusu Taratibu za Mchezo.

Klabu ya Stand United imeadhibiwa kwa kutozwa faini ya Sh. 1,000,000 (milioni moja) kwa kosa la mashabiki wake kumrushia mawe mwamuzi msaidizi namba moja wa mchezo tajwa hapo juu kwenye uwanja wa Kambarage, Shinyanga Julai 4, 2025.

Adhabu hii ni kwa mujibu wa kanuni ya 47:1 ya Championship kuhusu Udhibiti kwa Klabu.

Wachezaji Edgar Williams (Fountain Gate) na Selemani Richard Seif (Stand United) wamefungiwa michezo mitatu na kutozwa faini ya Sh. 500,000 (laki tano) kila mmoja kwa kosa la kukataa kuingia kwenye vyumba vya kuvalia wakati wa mapumziko na kusalia kiwanjani.

Wachezaji hao wawili walionekana kutegeana kila mmoja akisubiri mwenzake awe wa kwanza kuondoka kiwanjani jambo ambalo lilileta picha mbaya iliyotafsiriwa kama kitendo kinachoashiria Imani za kishirikina.

Adhabu hii ni kwa mujibu wa kanuni ya 41:5(5.5) ya Ligi Kuu na Kanuni ya 41:5(5.5) ya Championship kuhusu Udhibiti kwa Klabu.

SHAURI LA UHALALI WA WACHEZAJI WA TUNDURU KOROSHO

Timu ya Tunduru Korosho ya mkoani Ruvuma imetozwa faini ya Sh. 300,000 (laki tatu) na kupokwa ushindi wa jumla wa michezo miwili ya hatua ya mtoano dhidi ya Cargo FC ya Dar es Salaa, kuwania hadhi ya kucheza First League msimu wa 2025/2026 na timu ya Cargo kupewa ushindi pamoja na kupandishwa daraja kwenda First League 2025/2026, baada ya timu ya Tunduru kuthibitika iliwatumia wachezaji wawili ambao haikuwasajili.

Adhabu hii ni kwa mujibu wa kanuni ya 48:23 ya First League kuhusu Udhibiti kwa Klabu.

Kocha mkuu wa klabu ya Tunduru Korosho, Ramadhan Kadunda amefungiwa kwa kipindi cha mwaka mmoja na kutozwa faini ya Sh. 500,000 (laki tano) kwa kosa la kuwachezesha wachezaji wawili ambao hawakusajiliwa na klabu hiyo kwa ajili ya msimu wa 2024/2025.

Adhabu hii ni kwa mujibu wa kanuni ya 46:2(2.10) ya First League kuhusu Udhibiti kwa Makocha.

Katibu mkuu wa klabu ya Tunduru Korosho, Hassan Issa amepelekwa kwenye Kamati ya Maadili ya TFF kwa tuhuma za kughushi nyaraka za TFF zikiwemo leseni za wachezaji wawili waliotumika katika michezo tajwa hapo juu isivyo kihalali.

Mratibu (GC) wa mchezo tajwa hapo juu, Mkwenya Manya amepelekwa kwenye Kamati ya Maadili ya TFF kwa kosa la kuchelewa kwa makusudi kutuma nyaraka (picha za leseni za wachezaji) zilizoombwa na Bodi ya Ligi Kuu Tanzania, jambo ambalo limetafsiriwa kama hila za kuficha udanganyifu uliofanywa na klabu ya Tunduru Korosho.

Wachezaji Miraji Mohamed Daud na Oscar Stuati Omari wa klabu ya TANESCO ya mkoani Iringa, wamefungiwa kwa kipindi cha mwaka mmoja kwa kosa la kuitumikia klabu ya Tunduru Korosho katika michezo ya hatua ya mtoano wakiwa wanafahamu kuwa wao si wachezaji halali wa klabu hiyo.

Adhabu hii ni kwa mujibu wa kanuni ya 48:23 ya First League kuhusu Udhibiti kwa Klabu.