Abidjan. Mshindi wa mashindano ya Kimataifa ya Quran Tukufu 2024 Ibrahim Sow (17) raia wa Ivory Coast ameripotiwa kufariki dunia Jumanne Julai 15, 2025 nchini Ivory Coast.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka tovuti mbalimbali za habari nchini humo zinaeleza kuwa Sow alifariki, baada ya kuugua ghafla ingawa familia haijatoa maelezo rasmi kuhusu chanzo kamili cha kifo chake.
Sow alijizolea umaarufu mkubwa mwaka 2024 baada ya kuibuka mshindi wa kwanza katika mashindano ya kimataifa ya usomaji wa Qur’an yaliyofanyika jijini Dar es Salaam.
Ushindi huo ulimuwezesha kushinda Sh27 milioni ambazo alikabidhiwa na Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi.
Umahiri wake katika kuhifadhi na usomaji wa Qur’an tukufu vilimpa heshima na umaarufu si tu barani Afrika bali pia katika jumuiya mbalimbali za Waislamu duniani.
Baada ya kutangazwa kwa kifo chake kupitia mitandao mbalimbali ya kijamii, watu kutoka mataifa mbalimbali wametoa salamu zapole huku wakieleza namna alivyokuwa mfano wa kuigwa kwa vijana.