Camara akitoka tu, hawa wanatua

SIMBA ina hesabu kali ya kufumua eneo la kipa na unaweza kusema hakuna aliye salama, mezani kwa mabosi wa klabu hiyo kuna majina ya makipa wawili wanasubiri maamuzi tu, ili kuchukua nafasi ya Moussa Camara, iwapo wataamua kumpiga chini.

‎Camara aliyetua Simba msimu wa 2024/25 na kupata nafasi ya kucheza kama kipa namba moja muda wote, alisaini mkataba wa mwaka mmoja wenye nafasi ya kuongezeka na taarifa za awali kutoka ndani ya Simba zilikuwa zikidaiwa huenda akapigwa chini kabla ya mabosi hao kubadilika waendelee naye.

‎Taarifa za ndani zililiambia Mwanaspoti kuwa bado Camara hayupo salama, licha ya kufanya kazi nzuri kwenye msimu wake wa kwanza ndani ya Simba.

‎‎Ripoti ya makocha wa kikosi hicho ilieleza kuwa, kama atapatikana kipa mwenye ubora zaidi ya Camara, basi mabosi hao watafanya maamuzi na sasa kuna makipa wawili.

‎Jina la kwanza ni kipa wa Al Hilal ya Sudan, Issa Fofana ambaye awali aliwaambia mabosi wa Simba kwamba amemaliza mkataba, lakini baadae ikaja taarifa kuwa raia huyo wa Ivory Coast, bado ana mkataba.

‎‎Fofana ni kipa imara ambaye msimu uliopita amekuwa na rekodi nzuri, Simba inataka kupata ubora wake lakini pia uzoefu wake ili kuimarisha eneo hilo.

‎‎Kitu pekee ambacho Simba inakipigia hesabu ni namna Al Hilal itakubali kumuachia kipa huyo aliyefanya vizuri kwenye Ligi ya Mauritania, ambako Wasudan hao walishiriki kwa kibali Maalum kufuatia machafuko ya nchini kwao.

‎‎Kipa wa pili ni Drisa Bamba, ambaye ni raia wa Ivory Coast pia amemaliza mkataba na klabu ya Stade d’abidjan ya kwao kwa mafanikio.

‎‎Tetesi zinasema kuwa; “Simba inaona itanufaika na uzoefu wa Bamba akiwa na ubora wa kuwa nahodha kwenye klabu anazotoka.

‎‎”Mabosi hao wamefanya mazungumzo na Bamba na kugundua kwamba kipa huyo anaweza kuongea kiingereza vizuri na Kifaransa, ambapo itakuwa faida kwao kwenye mawasiliano na wenzake uwanjani.

‎‎Kiongozi mmoja wa Simba aliliambia Mwanaspoti; “Unajua mchakato imesimama kidogo tunamsubiri Mwenyekiti wa Bodi ambaye msimu huu anataka kuwa sehemu ya kufanikisha usajili hasa kwenye maamuzi.

‎‎”Kama tutakubaliana kumtoa Camara basi mmoja kati ya hao ndio atachukua nafasi yake lakini Camara akibakizwa, mchakato huo utaishia hapo.”

Camara ambaye alitua Simba Julai 30,2024 mpaka kufikia tarehe hiyo mwezi huu, mkataba wake utakuwa umemalizika hivyo Simba inakazi ya ziada ya kufanya maamuzi kabla ya huo muda kama haimhitaji msimu ujao.

Taarifa za ndani zililiambia Mwanaspoti; “Kipa huyo bado hajapewa mkono wa kwa heri na mabosi wa klabu hiyo, hivyo hadi Julai 30 kama atakuwepo basi maana yake bado ni mchezaji wa Simba.