INEC yaonya, ikielekeza wasimamizi kutokuwa chanzo cha malalamiko

Njombe/Moshi. Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) imewataka waratibu wa uchaguzi, wasimamizi na maofisa ununuzi kuhakikisha wanatunza vifaa vya uchaguzi kwa uangalifu mkubwa na kuepuka kuwa chanzo cha malalamiko kutoka kwa vyama vya siasa vitakavyoshiriki Uchaguzi Mkuu wa Wabunge na Madiwani utakaofanyika Oktoba 2025.

Kauli hiyo imetolewa leo Alhamisi, Julai 17, 2025 na ofisa wa INEC, Daniel Kalinga kwa niaba ya Mwenyekiti wa Tume hiyo, Jaji Jacob Mwambegele wakati wa kufunga mafunzo kwa waratibu wa uchaguzi wa mikoa ya Njombe, Iringa na Ruvuma yaliyofanyika mkoani Njombe.

Ofisa kutoka INEC Daniel Kalinga akifunga mafunzo kwa waratibu wa uchaguzi wa mikoa ,wasimamizi wa uchaguzi na maafisa ununuzi kutoka mikoa ya Njombe, Iringa na Ruvuma yaliyofanyika kwa siku tatu huko mkoani Njombe.



Kalinga amesema ni wajibu wa wasimamizi kuhakikisha wanahakiki vifaa vya uchaguzi baada ya kukabidhiwa na iwapo watabaini upungufu wowote, watoe taarifa haraka katika ofisi za Tume kwa ajili ya hatua stahiki.

Aidha, amesisitiza umuhimu wa usimamizi makini wa matumizi ya fedha zitakazotolewa kwa ajili ya maandalizi na utekelezaji wa uchaguzi huo, akisema:

“Ni muhimu kuhakikisha fedha hizo zinatumika kwa ufanisi na kwa mujibu wa taratibu zilizowekwa ili kufanikisha uchaguzi kwa mafanikio.”

Kalinga pia amewataka wasimamizi hao kuwa waelimishaji bora kwa wasimamizi wasaidizi wa ngazi ya kata na watendaji wa vituo vya kupigia kura, wakitekeleza jukumu hilo kwa weledi mkubwa.

Kwa upande wake, mwakilishi wa INEC, Phina Kidunda amesema jumla ya washiriki 145 kutoka mikoa ya Njombe, Iringa na Ruvuma wamepatiwa mafunzo hayo ya kitaalamu yaliyolenga kuwawezesha kusimamia uchaguzi kwa mujibu wa sheria na miongozo ya tume.

Mwakilishi kutoka INEC Phina Kidunda akizungumza na waratibu wa uchaguzi wa mikoa ,wasimamizi na maafisa ununuzi kutoka mikoa ya Njombe, Iringa na Ruvuma.



Amewakumbusha washiriki hao kuzingatia viapo vyao na kuwataka wakawe chachu ya kuzingatia Katiba, sheria, kanuni, miongozo na maelekezo yote waliyoelekezwa na waepuke mienendo inayoweza kuwa kikwazo au sababu ya malalamiko kutoka kwa wagombea na wadau wa uchaguzi.

Mratibu wa Uchaguzi Mkoa wa Iringa, Nuru Sovela kwa upande wake amesema mafunzo hayo yamewapa uelewa wa kina kuhusu majukumu yao na yatawawezesha kusimamia mchakato wa uchaguzi kwa kufuata sheria, kanuni na miongozo iliyowekwa na Tume.

“Vyama vya siasa vinapaswa pia kuzingatia sheria na miongozo ya tume ili kuhakikisha uchaguzi unafanyika kwa haki na utulivu,” amesema Sovela.

Naye Mratibu wa Uchaguzi wa Jimbo la Njombe Mjini, Samson Medda, ameahidi kutekeleza majukumu yake kwa uadilifu, akisema:

“Tutaishi viapo tulivyoapa na kufuata matamko rasmi. Hii itatusaidia kufanya kazi kwa weledi, kwa kufuata sheria na kuepuka ukiukwaji wa kanuni za uchaguzi.”

Wakati huo huo; kutokea Moshi mkoani Kilimanjaro, waratibu na wasimamizi wa uchaguzi kutoka mikoa ya Kilimanjaro na Tanga wametakiwa kupunguza makundi sogezi ‘Whats App’ katika kipindi hiki cha kuelekea kwenye uchaguzi mkuu, ili kuepuka kuvujisha taarifa za siri kwa kutuma sehemu isiyostahili.

Mbali na hilo pia waratibu hao na wasimamizi wametakiwa kuzingatia kiapo cha kutunza siri na kutambua kuwa, kutoa taarifa za siri bila ruhusa ni kosa la kisheria litakalowafanya wawajibishwe.

Rai hiyo imetolewa leo, Julai 17, 2025 na Mjumbe wa Tume huru ya Taifa ya uchaguzi, Dk Zakia Abubakar wakati akifunga mafunzo ya siku tatu kwa waratibu wa uchaguzi wa mkoa, wasimamizi na wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi ngazi ya majimbo, maofisa uchaguzi na maofisa ununuzi kutoka mikoa ya Kilimanjaro na Tanga yaliyofanyika mjini Moshi.

Amesema katika kipindi hiki cha uchaguzi yapo makundi sogozi mengi, hivyo ni vyema wakayapunguza ili kuepuka kukosea na kutuma taarifa ambazo hazikustahili kutumwa katika makundi hayo.

“Hivi sasa yapo makundi sogezi ya Whats App, jitahidini katika kipindi hiki muyapunguze ili msije kukosea kutuma taarifa ya aina yoyote katika makundi hayo ambayo haikutakiwa kutumwa huko,” amesema Dk Zakia

Mjumbe wa Tume huru ya Taifa ya uchaguzi, Dk Zakia Abubakar  akizungumza wakati wa kufunga mafunzo kwa waratibu na wasimamizi wa uchaguzi kutoka mkoa wa Kilimanjaro na Tanga



Amewakumbusha kuwa kabla ya kuanza mafunzo waliapa kuwa watatunza siri. “Kiapo hicho kipo kwa mujibu wa kanuni za uchaguzi wa Rais, wabunge na madiwani ya mwaka 2025.Ukiukwaji wa kiapo hicho kwa kuanza kutoa taarifa za siri ambazo tume haikukupa maelekezo ya kuzitoa katika utekelezaji wa kazi zake maana yake utakuwa umetenda kosa chini ya sheria na utawajibika kwa kosa hilo.”

Katika hatua nyingine, amesema  katika uboreshaji wa Daftari la Kudumu la wapiga kura, imebainika  changamoto ya kutobandikwa kwa mabango na matangazo ya  kuelekeza aliyekuwa na sifa za kuandikishwa na wadau wengine kufika kilipo kituo na kuwaagiza kuhakikisha changamoto hizo hazijitokezi kipindi hiki cha mchakato wa uchaguzi.

“Natumia nafasi hii kuwahimiza kuwa ubandikaji wa mabango, matangazo na orodha ya majina ni kwa mujibu wa sheria na kanuni zinazosimamia uchaguzi hivyo ni wajibu wenu kuhakikisha mabango, matangazo na orodha ya majina vyote vinavyotakiwa vinabandikwa kulingana na kalenda ya utekelezaji wa majukumu ya uchaguzi,” amesema.

Dk Zakia pia amewakumbusha waratibu hao kuhakikisha wanapokea na kuhakiki vitambulisho na barua za utambulisho za taasisi au asasi zitakazotoa elimu ya mpiga kura au kuwa waangalizi wa uchaguzi. Amesisitiza kuwa ni lazima kuhakiki kama wameidhinishwa na tume na wamepangiwa katika maeneo husika.

“Ikiwa utabaini kuwa mwangalizi hajapangiwa katika jimbo lako, wasiliana haraka na tume. Pia, si jukumu lenu kusindikiza asasi kwenye maeneo ambayo hawakuruhusiwa kufika,” amesema.

Kaimu Mkurugenzi wa Uchaguzi INEC, Dk Rose Likangaga



Kaimu Mkurugenzi wa Uchaguzi INEC, Dk Rose Likangaga amesema ujuzi na mbinu walizozitoa kwa wasimamizi hao  zitawasaidia kutekeleza vyema jukumu la uchaguzi siku zijazo.