Bugando yawafanyia upasuaji rekebishi wa uso, shingo wagonjwa 100

Mwanza. Zaidi ya wagonjwa 100 waliokuwa wakikabiliwa na changamoto za kimaumbile kwenye uso, shingo na kichwa wamepata huduma za upasuaji sanifu na rekebishi katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda Bugando.

Huduma hizo zimetolewa kupitia kambi maalumu za upasuaji kwa kushirikiana na wataalamu wa upasuaji kutoka Marekani tangu mwaka 2023, zikileta matumaini kwa wananchi waliokuwa wakikosa huduma hizo kutokana na uhaba wa wataalamu waliobobea nchini.

Katika awamu ya tano ya kambi hiyo iliyoanza Julai 14 na kuhitimishwa Julai 18, 2025 jumla ya wagonjwa 40 wenye changamoto za uso kuharibika kwa mashambulizi ya bakteria, pua zilizoharibika kutokana na ajali, na mdomo wazi walifanyiwa upasuaji rekebishi.

Hayo yameelezwa leo Alhamisi Julai 17, 2025 na Mkuu wa Idara ya Upasuaji Sanifu na Rekebishi Bugando, Dk Francis Tegete, alipotoa tathmini ya kambi hiyo ya wiki moja mbele ya waandishi wa habari.

Amesema kambi hiyo inalenga kutoa huduma kwa wananchi wenye changamoto za kuzaliwa nazo, ajali, saratani na mashambulizi ya bakteria kwenye maeneo ya uso, shingo na kichwa.

“Tumeanza kambi yetu Jumatatu tutamaliza Ijumaa, mpaka sasa tumewaona wagonjwa 35 na tunategemea hadi Ijumaa wataongezeka kwa sababu malengo yetu ni kuwaona wagonjwa 40 ambao wote watapatiwa huduma za kibingwa bobezi na timu tunashirikiana nayo,” amesema Dk Tegete.

Dk Tegete amesema idara yake hufanya kati ya upasuaji 80 hadi 130 kwa mwezi na kuangalia wagonjwa wa nje zaidi ya 300, wengi wakiwa na changamoto za majeraha ya moto, ajali, mdomo wazi, saratani na urembo.

Amesema kambi hizo zimekuwa muhimu kwani zimeongeza uwezo wa madaktari wa ndani kufanya oparesheni hizo hata baada ya wataalam kutoka Marekani kuondoka.

“Timu yetu imeimarika kwa kupata wataalamu wengi, pia huduma hii imepunguza mzigo kwa wananchi ambao wangelazimika kwenda nje ya nchi kwa matibabu zaidi,” amesema Dk Tegete.

Kiongozi wa timu ya wataalam kutoka Chuo cha American Plastic Surgery, Profesa Dk Manoj Abraham, amesema malengo ya programu ya Face to Face ni kutoa mafunzo kwa madaktari wa ndani ili kutoa huduma zenye kiwango sawa na Marekani.

“Kambi yetu inaendelea vizuri wagonjwa tuliowafanyia upasuaji wanaendelea vizuri na wanafurahia matokeo. Tunataka kuendeleza ushirikiano huu ili kujenga uwezo mkubwa wa kitaalam,” amesema Profesa Abraham.

Naye, Dk Gustave Buname, Daktari wa upasuaji wa masikio, pua na koo amesema: “Kwa miaka mitatu tumeona mabadiliko makubwa, sasa tunaweza kuhudumia hadi wagonjwa 12 kwa siku kutoka watatu wa awali.”

Paschalia John, mkazi wa Igoma, Mwanza, amepongeza huduma hizo akisema mtoto wake anayeendelea na huduma ya kunyooshwa viungo ameonyesha maendeleo makubwa.

“Nilimleta mwanangu akiwa hajiwezi lakini kwa sasa anaendelea vizuri na nawapongeza madaktari kwa kazi yao kubwa,” amesema Paschalia.