HUENDA hii isiwe taarifa njema kwa mashabiki wa klabu ya Simba, lakini inadaiwa hali ndivyo ilivyo, baada ya mabosi wa Yanga kufanya umafia wa aina yake kwa beki wa kushoto wa Msimbazi, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’.
Nyota huyo mwandamizi na nahodha wa Simba alyeitumikia timu hiyo kwa zaidi ya misimu 10 tangu aliposajiliwa kutoka Kagera Sugar mwaka 2014, amemaliza mkataba wa Wekundu hao na kwa bahati mbaya mabosi wa klabu hiyo walishindwa kumpa mkataba mpya mapema.
Mara paap, Yanga wakaamua kumfuatilia hasa baada ya kupitia ripoti ya aliyekuwa kocha mkuu wa timu hiyo, Miloud Hamdi aliyepo Ismalia ya Misri, aliyependekeza aongezwe beki wa kushoto mzawa na ilipoibuka suala la Tshabalala kutopewa mkataba mpya wa kuitumikia Simba wakaamua kujiongeza.
Inadaiwa kuwa, beki huyo ameshamalizana na Yanga baada ya mabosi wa klabu aliyoitumikia kwa zaidi ya misimu 10 kushindwa kuafikiana naye dili jipya.
Beki huyo wa kushoto aliyetua Msimbazi mwaka 2014 akitokea Kagera Sugar amemaliza mkataba na Simba na hakufanya mazungumzo yoyote mapema hadi baada ya msimu kumalizika na inadaiwa mabosi wa klabu hiyo walitaka kumpa dau dogo kuliko alilolitaka, hivyo naye akafanya uamuzi mgumu.
Taarifa za kuaminika zilizoifikia Mwanaspoti baada ya jana kuripoti klabu kongwe za Simba na Yanga pamoja nyingine kutoka Uarabuni zilikuwa zikichuana kuisaka saini yake, zinadai beki huyo zao la Azam FC amemwaga wino Jangwani akipewa mkataba wa miaka miwili.
Chanzo hicho kilisema Yanga ilimtumia Tshabalala mkataba akiwa katika majukumu ya timu ya Taifa, Taifa Stars iliyopiga kambi huko Misri ikijiandaa na fainali za ubingwa kwa nchi za Afrika (CHAN) 2024 zitakazofanyika Tanzania ikishirikiana na Kenya na Uganda, naye inadaiwa akamaliza mambo.
“Viongozi wa Yanga walimtumia mkataba Tshabalala akiwa kambini na kausaini siku chache nyuma na tayari kaurejesha, hivyo ni suala la muda kumtangaza kuwa sehemu ya kikosi chao msimu uliopita,” kilisema chanzo hicho na kuongeza;
“Simba nayo ilianza kuzungumza naye kabla ya kuondoka nchini, lakini walishindwana baada ya kuelezwa hatapewa kile anachokitaka kwa vile umri umeenda, ndipo akaamua kufuta hadi utambulisho wake wa Simba na akatimka na Stars bila kuupokea mkataba.
“Ishu ilikuwa ni dau la usajili, halikufikia kile mchezaji anachotaka, hivyo akaamua kuchukua pesa ndefu kwa ajili ya maisha yake, soka ni la muda mfupi mwishowe akianza kuombaomba watamcheka. Kama hujui Tshabalala alitoa muda mrefu kwa Simba kufanya kile anachokihitaji, lakini ikaonekana kama hawazingatii jambo hilo.”
Mwanaspoti likawatafuta watu wa karibu wa mchezaji ili kujiridhisha na hilo na mmojawao alijibu: “Hilo linawezekana kwa asilimia kubwa zaidi, kulionekana hakuna maelewano mazuri na Simba na kiongozi wa mchezaji kaonekana katika ofisi ya tajiri mmoja wa Yanga, mchezaji mwenyewe tayari katoa utambulisho wa mchezaji wa Simba katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii Instagram.”
Tshabalala ameondoa utambulisho huo baada ya miaka zaidi ya 10 tangu ajiunge na timu hiyo msimu wa 2014 ilipomsajili akitokea Kagera Sugar na kupita mikononi mwa makocha 16, mkataba wake na Wekundu hao umemalizika mwisho wa msimu huu.
Iwapo dili hilo litakuwa limetiki kama inavyodaiwa, Tshabalala huenda ataenda kuunda ukuta wa Yanga utakaoongozwa na kipa Diarra Djigui, Israel Mwenda, Dickson Job na Ibrahim Bacca, mbali na mabeki wanaosubiri nje kama Kibwana Shomary, Yao Kwasi, Chadrack Boka na Bakar Mwamnyeto.
Kama Tshabalala kamwaga wino, ina maana anakuwa mchezaji wa tatu kutua Jangwani baada ya kiungo Mohamed Doumbia na Celestin Ecua kwa ajili ya kuitumikia timu hiyo msimu ujao.
Akiwa na jezi ya Simba, Tshabalala ametwaa mataji mengi ikiwamo ubingwa wa Ligi Kuu Bara mara nne, Ngao ya Jamii mara tano, Kombe la Muungano mara moja.
Pia ameisaidia Simba kufanya vizuri katika michuano ya CAF akiifikisha robo fainali ya Ligi ya Mabingwa mara nne na Fainali ya Kombe la Shirikisho mara moja.
Bila kusahau umuhimu wake katika kikosi cha timu ya Taifa Stars amecheza fainali za Mataifa ya Afrika (Afcon) mara mbili kati ya tatu ambazo Stars imeshiriki.
Kama ameondoka Simba, ina maana timu hiyo imepoteza mabeki watatu wa pembeni waliokuwa nao msimu uliomalizika hivi karibuni akiwamo Valentin Nouma aliyekuwa akipokezana na Tshabalala sambamba na Kelvin Kijili aliyejiunga na Singida Black Stars, mbali na beki wa kati Hussein Kazi.