Serikali kununua ndege nne kudhibiti wadudu waharibifu

Morogoro. Katika juhudi za kukabiliana na changamoto ya uharibifu wa mazao na kuimarisha usalama wa chakula nchini, Serikali imepanga kununua ndege nne zitakazotumika kunyunyizia dawa za kuua wadudu waharibifu. Hatua hiyo inalenga kulinda mazao ya wakulima na kuongeza usalama wa chakula kinachozalishwa ndani ya nchi.

Akizungumza na Mwananchi leo Alhamisi, Julai 17, 2025, mjini Morogoro, Mkurugenzi wa Kitengo cha Ufuatiliaji na Tathmini kutoka Wizara ya Kilimo, Joseph Kiraiya amesema Serikali inaendelea kuwekeza katika sekta ya kilimo, hali inayochangia kuongeza uzalishaji wa chakula na kuboresha maisha ya wananchi.

Kiraiya ametoa kauli hiyo baada ya kufungua rasmi mafunzo kwa wataalamu wa ufuatiliaji na tathmini, yanayolenga kuwajengea uwezo katika kusimamia miradi ya maendeleo, hususan ile ya kilimo.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu, Dk Jim Yonaz amewataka wataalamu hao kuhakikisha wanatumia ipasavyo mafunzo hayo katika kuboresha mfumo wa ufuatiliaji wa miradi ya Serikali, hasa miradi ya kilimo inayotekelezwa maeneo mbalimbali nchini.

Dk Yonaz amesema idara ya ufuatiliaji na tathmini ni mpya, ni muhimu kwa wataalamu hao kuwa walimu kwa wengine na kusambaza elimu watakayokuwa wameipata katika maeneo yao ya kazi.

“Ni muhimu wataalamu wetu wawe na uwezo wa ziada katika kutekeleza majukumu yao. Mafunzo haya yawasaidie kuongeza ufanisi na uwajibikaji katika kazi za kila siku,” amesema.

Aidha, amesema baada ya kuidhinishwa kwa bajeti ya Serikali, miradi mingi ya maendeleo inaendelea kutekelezwa, hivyo wataalamu wa ufuatiliaji na tathmini wanatakiwa kwenda kusimamia miradi hiyo kwa weledi na kufanya tathmini ya kina ili kuhakikisha fedha za umma zinatumika kwa ufanisi na kwa manufaa ya wananchi.

“Lazima miradi ya Serikali ifanyiwe ufuatiliaji wa kutosha ili kuzuia upotevu wa fedha na kuhakikisha kila senti inayotolewa inaleta matokeo chanya kwa jamii,” amesema.

Hatua ya Serikali kununua ndege hizo ni sehemu ya mkakati mpana wa kuinua sekta ya kilimo nchini kwa kutumia teknolojia na kuongeza ufanisi katika kukabiliana na changamoto sugu zinazowakabili wakulima, ikiwemo wadudu waharibifu wa mazao.