Hijra ya Mtume tukio muhimu katika Uislam

Dar es Salaam. Kuhama (hijra) ya Mtume (Rehema na amani ziwe juu yake) kutoka Makka kwenda Madina ni miongoni mwa matukio muhimu zaidi katika historia ya Uislamu.

Haikuwa tu kuhama kutoka sehemu moja kwenda nyingine, bali ilikuwa ni hatua ya mabadiliko makubwa katika safari ya Uislamu na mwanzo wa kuasisiwa kwa Dola ya Kiislamu.

Hili tukio lilikuwa ni mwanzo wa kipindi kipya cha kisiasa, kijamii, na kidini katika historia ya Uislamu.

Kabla ya Hijra, mji wa Makka ulikuwa kituo kikuu cha biashara na dini katika rasi ya uarabuni. Ndani yake kulikuwapo Ka‘aba, nyumba ya Allah tukufu ambayo washirikina walitundika masanamu nadni yake, na ilikuwa makazi ya makabila makubwa ya Kiarabu yaliyokuwa na maslahi ya kiuchumi katika eneo hilo.

Mtume wa Allah alianza kueneza ujumbe wa Uislamu katika mji wa Makka, lakini alikumbana na upinzani mkali hasa kutoka kwa kabila kuu la Kuraishi.

Kwa sababu hiyo, Waislamu wa mwanzo waliteswa, wakanyanyaswa na kudhulumiwa sana, kiasi cha kufanya hali ya maisha yao ya Makka isiweze kuvumilika.

Katika mazingira hayo magumu, Mtume  wa Allah alianza kutafuta mahali salama pa kueneza dini ya Allah. Baada ya   ya makubaliano ya Aqaba ya pili (Bay‘atul-‘Aqabah) kati ya Mtume na kundi la watu kutoka Yathrib (Madina), aliwahimiza Waislamu wahamie Madina.

Hijra haikufanywa kiholela. Ilikuwa ni matokeo ya mipango ya kina na ya muda mrefu. Mtume wa Allah alichukua tahadhari zote zinazohitajika ili kuhakikisha usalama wake na wa Maswahaba wake.

Waislamu walianza kuhama mmoja mmoja kwa siri. Hatimaye, Mtume alihama mwenyewe pamoja na Abubakr As-Swiddīq (Allah amridhie). Katika safari hiyo, walitumia kila mbinu kuwadanganya adui zao Makuraishi, ikiwa ni pamoja na kujificha ndani ya pango la Thawr kwa siku tatu. Utafiti wa kisasa umeangazia Hijra kutoka mitazamo mbalimbali.

Watafiti huangalia sababu na vichocheo vya Hijra, pamoja na athari zake za kijamii, kisiasa, na kidini kwa muda mrefu, si tu katika Rasi ya Uarabuni tu, bali hata katika ulimwengu wa Kiislamu kwa ujumla.

Sababu na vichocheo vya Hijra

Sababu za kidini: Kulinda dini ya haki (Uislamu) kutokana na dhuluma za Makraishi. Kuwapa Waislamu wapya fursa ya kuabudu kwa uhuru. Kupanua wigo wa wito wa Uislamu kwa watu binafsi na makabila mbalimbali.

Sababu za kisiasa: Kuanzisha dola huru ya Kiislamu isiyodhibitiwa na makabila ya kishirikina ya Makka. Kuwezesha maendeleo ya jamii ya Kiislamu kwa uhuru wa kisiasa.

Sababu za kijamii: Kuweka mazingira salama kwa Waislamu wapya kuishi kwa utulivu na kuabudu kwa amani. Kuijenga jamii ya Kiislamu yenye mshikamano, usawa, na udugu baina ya watu wa makabila na matabaka tofauti.

Hijra ilisababisha kuanzishwa kwa dola ya kwanza ya Kiislamu huko Madina. Mtume aliweka Mkataba wa Madina, uliodhibiti uhusiano baina ya wakazi wa Madina, wakiwemo Waislamu, Wayahudi na washirikina.

Alianza kwa kuwaunganisha Muhajirina na Ansar kwa udugu wa Kiislamu, kisha akapanga uhusiano wa pamoja baina ya makundi yote katika jamii hiyo.

Baada ya kuunganisha undugu (mu’akhaat) baina ya Muhajirina na Ansar, athari za mshikamano zilianza kujitokeza wazi katika jamii mpya ya Kiislamu. Uhusiano wa karibu kati ya watu wa makundi haya mawili ulizidi kuimarika.

Hii iliimarisha mshikamano wa kijamii katika dola ya Kiislamu. Baada ya Hijra, Uislamu ulienea kwa kasi katika sehemu nyingi za Uarabuni na maeneo ya jirani. Madina ikawa kituo kikuu cha ulinganizi wa Kiislamu kwa makabila mbalimbali.

Mtume wa Allah alianzisha mfumo wa kipekee wa kisiasa na kijamii ambao ulifanya Dola ya Kiislamu kuwa mfano wa haki, huruma, na mshikamano wa kijamii.

Wasomi wa Kimagharibi na wa kisasa waliitazama Hijra kwa mitazamo tofauti, lakini wengi wao hawakuweza kupuuza umuhimu wake katika historia ya mwanadamu. Bernard Lewis (mwanahistoria wa Kimagharibi,
aliielezea Hijra kuwa ni “Mapinduzi ya kidini na kijamii” yaliyowabadilisha Waarabu kutoka kuwa makabila yaliyotengana hadi kuwa taifa lililoungana lenye lengo la pamoja.

Naye Montgomery Watt (mwanahistoria wa kimataifa), alisema Hijra ilikuwa ni hatua ya mabadiliko makubwa katika maisha ya Mtume Muhammad, kwani alihamia kutoka kuwa kiongozi wa kidini hadi kuwa kiongozi wa kisiasa nakKijeshi, jambo lililoweka msingi wa kuibuka kwa Dola ya Kiislamu.

 Kwa upande wake Karen Armstrong (mwandishi wa kike Mwingereza), alisema, “Hijra ilikuwa hatua muhimu katika kubadilisha Uislamu kutoka harakati ndogo ya kidini kwenda kuwa nguvu ya kijamii na kisiasa yenye ushawishi mkubwa duniani.”

 Ama John Esposito (profesa wa dini wa Marekani), aliangazia Hijra kama chimbuko la mabadiliko ya kijamii na kisiasa, na kusema kwamba, “Hijra iliweka mfano mpya wa uhusiano kati ya jamii mbalimbali, na kuufanya Uislamu kuwa dini ya kimataifa inayokubali utofauti wa kibinadamu.”

Itaendelelea katika toleo lijalo In Shaa Allah.  0712690822