Ofisa Mtendaji afariki dunia akidaiwa kunywa sumu ya panya

Shinyanga. Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Ulowa Namba Moja, Kata ya Ulowa, Wilaya ya Kipolisi ya Ushetu, mkoani Shinyanga, Juliana Mkumbo (35), amekutwa amefariki dunia ndani ya chumba alichokuwa amepanga, huku milango ya nyumba hiyo ikiwa imefungwa kwa ndani.

Tukio hilo lilibainika usiku wa Julai 16, 2025, baada ya watumishi wenzake kushindwa kuwasiliana na Juliana kwa siku mbili mfululizo. Kufuatia hali hiyo, waliamua kutoa taarifa katika Kituo cha Polisi Ulowa.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, Janeth Magomi, amethibitisha kutokea tukio hilo.

Ameeleza kuwa, baada ya polisi kufika katika nyumba aliyokuwa akiishi mtendaji huyo enzi za uhai wake, walilazimika kuvunja mlango wa chumba hicho kwani ulikuwa umefungwa kwa ndani.

Kamanda Magomi amesema kuwa baada ya polisi kuvunja mlango wa nyumba hiyo, walimkuta Juliana akiwa amelala kitandani akiwa amefariki dunia na kulikuwa na matapishi juu ya kitanda chake.

Ameongeza kuwa uchunguzi wa tukio hilo bado unaendelea, lakini kwa mujibu wa taarifa ya awali ya daktari, marehemu anadaiwa kuwa alikunywa sumu ya panya, jambo linaloonekana kuwa  lilisababisha kifo chake.

Amesema; “Hakuonekana kwa muda hivyo baada ya taarifa, polisi  walikwenda kuvunja mlango wakamkuta akiwa kitandani na kuna matapishi lakini amefariki dunia.

“Mwili wake umefanyiwa uchunguzi katika Hospitali ya Manispaa ya Kahama na taarifa za awali za daktari ni kwamba ilionekana amekunywa sumu ya panya,” amesema.

Aidha, Kamanda Magomi ametoa wito kwa wazazi na walezi kuwalea watoto wao katika maadili mema na hofu ya Mungu, ili kuwajengea misingi imara ya kiroho na kisaikolojia itakayowasaidia kukabiliana na changamoto mbalimbali za maisha.

Amesema kufanya hivyo kutasaidia kuzuia matukio ya watu kujitoa uhai na kuwaacha wapendwa wao katika huzuni na simanzi.

 Mmoja wa wakazi wa Ulowa ambaye aliwahi kuwa kiongozi wa eneo hilo na ambaye hakupenda jina lake litajwe, amesema kuwa waligundua tukio hilo usiku wa Julai 16, 2025, baada ya kutomuona kwa siku mbili mfululizo.

Amesema walipotoa taarifa kwa polisi, walifika nyumbani kwake, wakavunja mlango na kumkuta tayari amefariki dunia.

“Sisi tukio hili tuligundua jana usiku, japo alikuwa ndani kwa muda wa siku mbili,askari walikuja wakavunja mlango wa sebuleni na chumbani na ndipo walipomkuta amelala akiwa amejifunga kitenge tu,” amesema.

Amesema watumishi wenzake marehemu walijaribu mara kadhaa kumpigia simu yake ya mkononi, lakini kila mara ilionekana inatumika, na hata walipobadilisha namba bado ilionekana inatumika ndipo walipotoa taarifa polisi waliofika na kugundua tukio hilo.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kijiji cha Kangeme, Mlangani Mwele amekiri kutokea kwa tukio hilo na kwamba mwili wa marehemu ulichukuliwa saa nane usiku na kupelekwa Hospitali ya Manispaa ya Kahama kwa ajili ya uchuguzi.

“Ni kweli ndugu tuna msiba katika kijiji chetu hapa Kangeme, amefariki mtendaji wa kijiji jirani cha Ulowa Namba Moja, ila alikuwa anaishi Kijiji cha Kangame, amekutwa amefariki ndani kwake ila polisi walikuja na mwili wake umepelekwa hospitali ya Manispaa ya Kahama kwa ajili ya uchunguzi zaidi,” amesema