Maneno ya mwisho ya kusikitisha ya rubani wa ndege ya Air India Flight 171, kabla ya ajali mbaya iliyosababisha vifo vya watu 260, yamefichuliwa kupitia rekodi za kisanduku cheusi zilizopatikana kwenye eneo la tukio.
Kwa mujibu wa vyanzo vya habari vya Magharibi vilivyotangazwa na gazeti la Corriere della Sera, nahodha wa ndege hiyo, Captain Sumeet Sabharwal, alimkabidhi rasmi usukani rubani msaidizi, Clive Kunder, muda mfupi kabla ya kuondoka kwa ndege hiyo: “Ndege iko mikononi mwako,” alisikika akisema.
Ndege hiyo, aina ya Boeing 787, ilikuwa ikielekea London ikitoka Ahmedabad, India. Ilipata ajali dakika chache baada ya kuruka, saa 7:38:39 mchana, ikiwa angani kwa takriban sekunde 30 tu, kabla ya kupoteza nguvu na kuanguka kwenye eneo la makazi karibu na chuo cha udaktari. Ajali hiyo ilisababisha vifo vya abiria 241 waliokuwa ndani ya ndege na watu 19 waliokuwa chini.
Kwa mujibu wa taarifa ya awali kutoka Shirika la Uchunguzi wa Ajali za Ndege la India (AAIB), swichi za mafuta zilihamishwa kutoka hali ya ‘run’ hadi ‘cutoff’ sekunde chache baada ya kuruka. Hata hivyo, haijafichuliwa ni nani aliyefanya mabadiliko hayo.
Katika rekodi za mawasiliano ya rubani, Kunder alisikika akimhoji Sabharwal: “Kwa nini umefunga injini?” ambapo majibu yasiyoeleweka vyema yalirekodiwa, yakionyesha kukanusha: “Sikufanya hivyo.” Ripoti inaeleza kuwa Kunder alirudia swali hilo mara kadhaa, akionyesha kutokuwa na imani na majibu aliyoyapata.
Ingawa hakuna video ya moja kwa moja iliyoripoti ndani ya kokpiti kuonyesha nani aligusa swichi, sauti za rekodi zinapendekeza kuwa huenda ilikuwa kazi ya rubani mkuu, Sabharwal, aliyekuwa rubani anayesimamia (pilot monitoring), wakati Kunder akiwa anairusha ndege (pilot flying). Kulingana na jarida la The Wall Street Journal, swichi hizo zilihamishwa kwa mpigo wa sekunde moja kila moja, kabla ya kurejeshwa kwenye hali ya kawaida sekunde 10 baadaye lakini tayari nguvu za injini zilikuwa zimeshakatika.
Swichi za kudhibiti mafuta si rahisi kubonyeza kwa bahati mbaya; zina mfumo wa kufungwa unaohitaji kuvutwa juu kabla ya kubadilishwa, jambo linalozua maswali makubwa kuhusu sababu ya kuhamishwa kwa swichi hizo.
Dakika chache baada ya kuruka, kamera za usalama zilionyesha kifaa cha dharura kinachoitwa Ram Air Turbine (RAT) kikitoka, ishara ya kupotea kwa nguvu kutoka kwenye injini. Ndege ilipanda hadi futi 650 kabla ya kuanza kushuka, huku ikijaribu kuwasha injini upya, lakini haikupata muda wa kutosha kurejesha nguvu. Mmoja wa marubani alisikika akipiga kelele ya dharura: “MAYDAY! MAYDAY! MAYDAY!”
Ndege iligonga miti na bomba la moshi kabla ya kulipuka kwa moto na kuanguka kwenye jengo la chuo cha udaktari, likisababisha vifo vya karibu wote waliokuwemo na uharibifu mkubwa wa miundombuni.
Swichi zote za mafuta zilipatikana kwenye hali ya “run” baada ya ajali, ikionyesha kuwa marubani walijaribu kuzirejesha, lakini ilikuwa tayari imechelewa.
Mtaalamu wa usalama wa anga, Terry Tozer, aliliambia Sky News kuwa hali hiyo ilikuwa ajabu kupita kiasi. Alisema injini zilikuwa zimeanza kupata nguvu wakati ndege ikiwa chini sana, hivyo hazikuweza kuokoa hali hiyo.”
Wakati huo huo, Waziri wa Uchukuzi wa Anga wa India, Kinjarapu Ram Mohan Naidu, alisema kuwa ni mapema mno kutoa hitimisho kuhusu chanzo cha ajali: “Tusubiri ripoti ya mwisho,” alisema akiwaeleza waandishi wa habari.
Wachunguzi pia wanachunguza hali ya afya ya akili ya marubani hao. Nahodha mstaafu Mohan Ranganathan, mtaalamu wa usalama wa anga nchini India, aliiambia The Daily Telegraph kuwa mmoja wa marubani aliripotiwa kuwa na matatizo ya kiafya ya akili katika miaka ya karibuni, na alichukua likizo ya matibabu. Pia, inadaiwa kuwa Captain Sabharwal alikuwa amerejea kazini baada ya likizo ya msiba kufuatia kifo cha mama yake, lakini alithibitishwa kiafya na Air India kabla ya kurudi kazini.
Kampuni ya Air India imesema inashirikiana kikamilifu na mamlaka za uchunguzi katika mchakato huu, huku ripoti ya mwisho ikitarajiwa kutolewa ndani ya mwaka mmoja