Tabora. Mkazi wa Kijiji cha Shitage, Wilaya ya Uyui mkoani Tabora, Zainabu Ndeko (65) amelazwa katika Hospitali ya Manispaa ya Kahama mkoani Shinyanga, baada ya kushambuliwa na watu wasiojulikana.
Ndeko amejeruhiwa katika maeneo mbalimbali ya mwili wake, kufuatia shambulio hilo linalodaiwa kufanywa kwa kutumia silaha yenye ncha kali.
Taarifa zaidi kuhusu tukio hilo zinaendelea kufuatiliwa, huku vyombo vya usalama vikiendelea na uchunguzi ili kubaini wahusika na sababu ya shambulio hilo.
Akizungumza na Mwananchi leo Julai 18, 2025, Josephina Mihayo ambaye ni wifi wa Zainabu, amesema Ndeko alishambuliwa na watu wasiojulikana usiku wa kuamkia Julai 16, 2025, majira ya saa mbili usiku.
Alisema baada ya tukio alipelekwa katika zahanati ya Kijiji cha Shitage na kuandikiwa rufaa ya kwenda Hospitali ya Manispaa ya Kahama kwa matibabu zaidi.
“Nilipigiwa simu na majirani zake wifi, kwamba amekatwa mapanga mida ya saa mbili usiku, wakampeleka zahanati ya Shitage, muda mfupi tu wakanipigia tena wameambiwa aje huku Kahama, ndipo nikaenda nikamleta hapa, ni tukio baya kabisa hilia,” amesema.
Kwa upande wake, Mwanaidi Mauba, tabibu katika oodi namba tatu ya Hospitali ya Manispaa ya Kahama, ambapo Zainabu amelazwa, amesema kuwa walimpokea usiku wa kuamkia Julai 16, majira ya saa tatu usiku, akiwa katika hali mbaya na akiwa na majeraha makubwa.
Amesema walimuanzishia matibabu ya haraka na hali yake inaendelea vizuri, lakini mkono wake wa kushoto ulikatwa kabisa.
Kamanda wa Polisi mkoani Tabora, Richard Abwao, alipoulizwa na Mwananchi kuhusu tukio hilo, amesema taarifa hizo hazijafika ofisini kwake. Ameongeza kuwa anaendelea kuzifuatilia na kuahidi kutoa ufafanuzi zaidi baadaye.
“Tukio hilo bado halijaja ofisini kwangu labda nilifatilie, halafu nitalitolea taarifa baadaye,” amesema kamanda Abwao.