TPDC, kampuni ya Nigeria zakubaliana utafiti wa gesi, mafuta

Dodoma. Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) limesaini mkataba wa awali wa miezi tisa na kampuni ya First Exploration and Petroleum Development Company Ltd (First E and P) ya Nigeria kwa ajili ya kutafuta mafuta na gesi kwenye kitalu cha Mnazi Bay Kaskazini.

Lengo la mkataba huo ni kuweka rasmi mwongozo wa namna watakavyoshirikiana hususani katika utafutaji na uendelezaji, huku mategemeo yakiwa ni kufikia kwenye uzalishaji kutoka kwenye kitalu hicho, ambacho Serikali imekipatia TPDC ili ikiendeleze.

Akizungumza na waandishi wa habari kwenye hafla ya kutia saini mkataba huo leo Julai 18, 2025 jijini Dodoma, Mkurugenzi Mkuu wa TPDC, Mussa Makame amesema hadi sasa kuna kazi nyingi ambazo zimeshafanywa na shirika hilo kwenye kitalu hicho, na nyingine bado wanataka kuzifanya hususani hatua ya kuchoronga visima kwa ajili ya kutafuta mafuta au gesi katika eneo hilo.

Makame amesema mradi wa Mnazi Bay ni mkubwa kwa sababu unatokea kwenye eneo la bahari, hivyo lina kina kirefu, na mpaka sasa eneo linalotaka kuchimbwa lina kina chenye urefu wa mita 800, kwa hiyo ni mradi wenye gharama kubwa.

“Katika sekta ya mafuta na gesi, ni jambo la kawaida kushirikiana na wengine ili kupunguza au kugawana hatari zilizopo, kwa sababu kisima cha gesi kinakadiriwa kufikia gharama za Dola za Marekani 60 milioni ambazo ni sawa na Sh150 bilioni.

“Na pale unaweza kuchimba visima mpaka vitatu ili kuthibitisha kiwango cha gesi kilichopo, halafu utengeneze miundombinu ya gesi mpaka kuifikisha nchi kavu kwa ajili ya matumizi mbalimbali kwenye umeme, viwanda, majumbani na kwenye magari,” amesema Makame na kuongeza:


“Sasa, ili kupunguza hizo gharama na hatari ambazo tunazichukua, ni kawaida katika sekta hii kushirikiana na kampuni zaidi ya moja. Kwa hiyo hawa wenzetu kutoka Nigeria, kama mnavyofahamu ni nchi inayoongoza Afrika katika uzalishaji wa mafuta na gesi tangu miaka ya 1960, waliona kuna fursa hapa nchini, wakaja tukazungumza nao,” amesema Makame.

Mkurugenzi huyo amesema kitalu hicho kinategemewa kuwa na gesi nyingi, kwa hiyo manufaa makubwa kwenye uwekezaji huo ni upatikanaji wa gesi ambayo itakuja kutumika kwenye matumizi mbalimbali hususani kwenye uzalishaji wa umeme, viwandani, majumbani na kwenye magari.

Naye Kamishna wa Petroli na Gesi katika Wizara ya Nishati, Goodluck Shirima amesema makubaliano hayo ya awali kati ya TPDC na First E and P yanaweka misingi ya awali ya namna TPDC inaweza kushirikiana na kampuni hii katika utafiti wa mafuta na gesi Mnazi Bay.

Amesema Serikali imekuwa ikifanya jitihada za kuiwezesha TPDC kuwa shirika la mafuta lenye nguvu na lenye uwezo wa kuendeleza vitalu vyenye uwezekano wa kuwa na mafuta na gesi wenyewe au kwa kushirikiana na wadau ambao watakuwa na nguvu na uzoefu ili kupunguza na kugawana hatari na kuepusha shirika lisije likapata hasara kubwa pale litakapowekeza kwa kiwango kikubwa na lisifanikiwe kugundua nishati husika.

“Serikali imekusudia kuipatia TPDC vitalu takribani vitano vya kimkakati kikiwemo cha Mnazi Bay North ambapo jitihada za kuviendeleza zimeanza, pamoja na kazi zilizoanza kwenye kitalu kilichopo Lindi na Mtwara, ili kuangalia uwezekano wa uwepo wa mafuta na gesi kwenye kitalu kile,” amesema Shirima.

Ameitaka TPDC kuendeleza jitihada hizo ili rasilimali hizo zikipatikana ziweze kutatua changamoto mbalimbali ambazo Watanzania wanapambana nazo kila siku.

Shirika limesema vitalu vilivyopo hapa nchini ambavyo vimeshafanyiwa ugunduzi vipo vitatu kwenye bahari kuu, ambavyo ni Block 1, 2 na 4 ambavyo vina ugunduzi wa kampuni kutoka nje ya nchi, vyenye gesi inayofikia futi za ujazo trilioni 47.

Kamishna huyo amesema kuna vitalu vingine 26 ambavyo wanatarajia kuvitangaza mwishoni mwa mwaka huu, ili kuwaalika wadau mbalimbali waweze kushiriki.

Amesema vitalu hivyo ni vile ambavyo vipo kwenye miamba tabaka ambayo ni zaidi ya asilimia 60 ya nchi, ambapo vina uwezo wa kuzalisha mita za ujazo trilioni 57 za gesi, ambapo mita za ujazo trilioni 47 zinapatikana baharini na trilioni 10 nchi kavu.

Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya First E and P, Ademola Adeyemi-Bero amesema Tanzania imebarikiwa kuwa na gesi nyingi, na kwamba huu ndiyo mwanzo wa ushirikiano wa kampuni hiyo na Tanzania katika ugunduzi wa mafuta na gesi.

Amesema baada ya utafiti huo kuonyesha mafanikio kwenye kitalu cha Mnazi Bay, kampuni hiyo itaingia makubaliano ya kuchimba na kusambaza gesi kwa wananchi.