Hospitali iliyoanza kujengwa 1975, yaanza kutoa huduma

Dodoma. Ujenzi wa Hospitali ya Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere ya Mkoa wa Mara iliyoanza kujengwa mwaka 1975, imeanza kutoa hudumu huku ujenzi wake ukiwa umefikia asilimia 70 na unatarajiwa kukamilika miaka miwili ijayo.

Hospitali hiyo kuanza kutoa huduma, kunakamilisha safari ya ujenzi wake ulioanza mwaka 1975 chini ya Mwalimu Julius Nyerere na sababu za kuchelewa zimeelezwa kuwa ni “katika kuifanya kuwa na ubora mkubwa.”

Hospitali hiyo iliyopo eneo la Kwangwa, Manispaa ya Musoma, imeanza kutoa huduma tangu mwaka 2023 na kupunguza asilimia 70 ya rufaa zilizokuwa zikienda katika Hospitali ya Kanda ya Bugando iliyopo Mkoa wa Mwanza.

Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi ameyasema hayo leo Ijumaa Julai 17, 2025 jijini Dodoma wakati akielezea mafanikio ya Serikali ya awamu ya sita kwenye mkoa wake.

“Serikali ya awamu sita inakamilisha ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere iliyoanza kujengwa mwaka 1975. Hospitali hiyo ilianza kutoa huduma Julai mosi 2023 wakati ukamilishaji wa baadhi ya miundombinu ukiendelea,” amesema.

Amezitaja huduma za kibingwa ambazo zimeanza kutolewa ikiwa ni pamoja na kliniki ya pua, masikio na koo (ENT), kliniki ya hemophilia, huduma za radiolojia, usafishaji damu, vipimo vya CT Scan, wodi inayotoa huduma za watoto njiti (NICU) na huduma za tiba mtandao (Telemedicine).

Pia, amesema hospitali hiyo ambayo ujenzi wake umefikia asilimia 70, imeanza gesi tiba ya oksijeni kwa ajili ya kutoa huduma kwa wateja wanaohitaji huduma ya gesi tiba pamoja na kuhudumia vituo jirani.

Kanali Mtambi amesema wanatarajia utolewaji wa fedha ukiendelea kama hivi sasa, baada ya miaka miwili itakuwa imekamilika.

“Ni hospitali kubwa, ukienda hudhani kwamba uko katika hospitali, ni hospitali ya kisasa. Kwenye hospitali hii helkopta itatua katika roof (juu ya paa) palepale hospitali, kwa hiyo akishushwa ni kwenye machela na kupelekwa kuhudumiwa,” amesema.

Kanali Mtambi amesema mitambo iliyopo katika hospitali hiyo inatumia umeme mkubwa, hivyo Serikali kupitia Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (Temesa) inafanya maboresho.

Amesema uwekezaji katika huduma za afya umepunguza umbali wa wananchi kufuata huduma kutoka kilometa 15 mwaka 2020 hadi kilometa tano mwaka 2025.

Waliopisha ushoroba walipwa

Aidha, Kanali Mtambi amesema Serikali imetekeleza maamuzi yaliyofanywa tangu wakati wa ukoloni ambapo mwaka 1959 baada ya utafiti iliopendekeza kuunganisha Ghuba ya Speke (eneo la Kata ya Nyatwali) kuwa sehemu ya Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.

“Uamuzi huo ulitokana na umuhimu wa eneo hilo katika ikolojia ya hifadhi na baadaye mwaka 1974 Serikali iliifanya Ghuba ya Speke kuwa Pori Tengefu kwa tangazo la Serikali Namba 269. Hata hivyo, ulipaji wa fidia ili wananchi kupisha eneo hilo,umefanywa sasa,” amesema.

Amesema utekelezaji huo umwefanyika baada ya kulipa Sh59.52 bilioni ikiwa imejumuishwa nyongeza ya asilimia saba kama fidia ya kuchelewa baada ya kufanyiwa tathmini.

Kanali Mtambi amesema shughuli hiyo imefanyika kwa amani na utulivu na tayari wafidiwa wamehama katika eneo hilo baada ya kupokea stahiki zao kwa mujibu wa sheria.

Amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa niaba ya wananchi wa Kata ya Nyatwali, kwa kulipa fidia kwa wananchi na Serikali kulitwaa eneo hilo la ushoroba wa wanyama wanaopita kwenda kunywa maji katika Ziwa Victoria.

Amesema kwa kuondolewa katika eneo hilo wananchi wameondokana na adha ya kuvamiwa na wanyama na kusababisha kupoteza maisha, kujeruhiwa na mazao yao kuvamiwa na wanyama mara kwa mara.

Wakati huohuo, Kanali Mtambi amesema mradi wa kupanga, kupima na kumilikisha ardhi kupitia Wizara ya Nyumba na Maendeleo ya Makazi umesaidia wananchi kuimarisha usalama wa miliki zao.

Amesema mradi huo umepunguza migogoro ya ardhi kutoka 964 mwaka 2020 hadi migogoro 125 mwaka 2025 na kuwawezesha wananchi kupata mikopo kutoka katika taasisi mbalimbali za kifedha.

Mapema, Ofisa wa Habari Idara ya Habari Maelezo, Kelvin Kanje ameeleza umuhimu wa mikutano kama aliofanya Mtambi, akisistiza kuwa inafuatiliwa na wananchi wanaotaka kufahamu ni mafanikio yaliyopatikana kwenye awamu ya sita kwenye mikoa yao.