SERIKALI YAWAONDOA HOFU WAZAZI KUHUSU MTAALA MPYA WA ELIMU MSINGI 2027…

NA WILLIUM PAUL, ROMBO.

SERIKALI imejipanga kikamilifu kutekeleza mikakati ya kuhakikisha wanafunzi wanaomaliza darasa la saba (mtaala wa zamani) na wale wa darasa la sita (mtaala mpya) mwaka 2027 wanaendelea na masomo bila vikwazo.

Hayo yamebainishwa na Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda jana, wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya mfumo wa kidijitali wa uthibiti ubora wa shule za msingi na sekondari wilaya ya Rombo, mkoani Kilimanjaro, ambapo alisema Serikali itatumia mbinu mbalimbali kuhakikisha hakuna mwanafunzi atakayeachwa.

Profesa Mkenda, amesema mwaka 2027 utakuwa wa kipekee, kwani kutakuwa na mahafali ya wanafunzi kutoka madarasa mawili tofauti, darasa la saba kwa mtaala wa zamani na darasa la sita kwa mtaala mpya ambao wote watamaliza elimu ya msingi kwa pamoja.

“Tutatumia mikakati ya aina mbalimbali kuhakikisha tunalitekeleza hili la elimu 2027 tuna mikakati ya akiba, tunajenga VETA kila Wilaya, tunaweza kufanya VETA ziache kuchukua wanafunzi kwa muda kwamba darasa la Saba na la Sita wote wanahitimu wakati mmoja , VETA ikawa Sekondari wakasoma kule wakimaliza VETA ikarudi kwenye shughuli zake,” alisema Profesa Mkenda

Alisema hatua nyingine ni kuzitumia baadhi ya shule za Sekondari za watu binafsi kupeleka watoto wa serikali, kwa kuwalipia ada endapo makubaliano ya ada yatakuwa ni mazuri ili wasome.