WAKATI Dodoma Jiji ikidaiwa kumalizana na aliyekuwa kiungo wa Tabora United, Mkongomani Nelson Munganga, mabosi wa timu hiyo wameanza harakati za kusaka mbadala wake, ambapo imetua kwa Mcameroon, Palai Mba Manjie ili kurithi mikoba yake.
Manjie anayeichezea Victoria United ya Cameroon kwa sasa, inadaiwa wawakilishi wa mchezaji huyo wametua tayari jijini Dar es Salaam, kwa ajili ya kufanya mazungumzo ya kumuuza, ambapo dili hilo la kiungo huyo linaendelea vizuri.
Kiungo huyo aliyezaliwa Mei 15, 2001, ni chaguo la kwanza la Tabora katika eneo la kiungo wa kati ili kuzipa nafasi ya Munganga anayedaiwa kumalizana na Dodoma Jiji, ambapo aligomea mkataba mpya na kuamua kutafuta changamoto sehemu mpya.
Mwanaspoti limedokezwa, mabosi wa Tabora wako Dar es Salaam kwa ajili ya kufanya mazungumzo na baadhi ya wachezaji ambao tayari wametumiwa na mawakala, hivyo, mchakato wa kuinasa saini ya Manjie unaendelea kimyakimya katika moja ya hoteli.
Hata hivyo, Mwanaspoti limepenyezewa taarifa mabosi wa Tabora wanafanya mazungumzo na nyota wengi wa kigeni hasa wale wa Nigeria, ambapo mmoja wa kigogo huyo alisema wachezaji wapo katika moja ya hoteli iliyopo Ukonga jijini Dar es Salaam.
“Siwezi kukutajia hiyo hoteli lakini fahamu tu ipo Ukonga na ndipo ambapo tunafanya mazungumzo na wachezaji na kama kila kitu kitaenda sawa kwa maana ya kupitishwa na benchi letu la ufundi tutawasainisha rasmi mikataba,” alisema kigogo huyo.
Kiongozi huyo alisema kuanzia wiki ijayo wataweka wazi majina kamili ya nyota wapya waliowasajili na wale wengine ambao watawapa mkono wa kwaheri, huku suala nzima la maandalizi ya msimu yaani ‘Pre Season’, likifanyiwa pia kazi taratibu.