Mashujaa kunoa makali Arachuga | Mwanaspoti

WAKATI timu zikisaka maeneo ya kwenda kufanya maandalizi kwa ajili ya msimu ujao, kikosi cha Mashujaa mapema imeshajua ni wapi itakwenda kuweka kambi yake.

Akizungumza na Mwanaspoti alisema mmoja wa viongozi wa klabu hiyo alisema, zipo sababu kama mbili ambazo zimewafanya waichague Arusha kama sehemu ya maandalizi yao.

“Tumekubaliana kwenda Arusha kwa ajili ya kambi ya maandalizi ya msimu mpya, kuna sababu kama mbili za uamuzi huu licha ya kwamba kuna maeneo mengi mazuri,” alisema kiongozi huyo na kuongeza;

“Sababu ya kwanza ni hali ya hewa, makocha wameshauri tukaweke kambi eneo ambalo kutakuwa na hali ya hewa ya baridi, inasaidia wachezaji kujiandaa vizuri kwenye miwili yao, tuliangalia maeneo mbalimbali kama Mbeya, Iringa lakini tukaona Arusha ni sahihi zaidi.

“Sababu ya pili ni uwepo wa nafasi ya kupata mechi za kirafiki, kuna timu nyingi zitakwenda Arusha, hivyo itatupa nafasi ya kupata mechi za kirafiki.”

Maandalizi ya timu kadhaa yatakwenda kufanyika Arusha, Mwanaspoti iliandika miongoni mwa klabu ambazo zimejipanga kwenda Mkoa huo ni pamoja na Singida Black Star.

Mashujaa itaendelea msimu ujao na kocha Salum Mayanga ambaye aliridhi mikoba kwa Abdallah Mohamed ‘Bares’ kutoka Machi 2025, wakati kikosi hicho kikielekea kwenye mechi dhidi ya Pamba katika michuano ya Kombe la FA.

Wazee hao wa mapigo na mwendo walimaliza msimu wakiwa nafasi ya saba katika mechi 30 ilizocheza,ikivuna pointi 35,ikishinda mechi nane,sare 11 na kupoteza 11.