Mnigeria ataka Sh250 milioni atue Tabora United

WAKATI Tabora United ikiwa katika mazungumzo ya kumsajili mshambuliaji wa Nasarawa United, Mnigeria Anas Opkadibu Yusuf Ayitonu, klabu hiyo inatakiwa kulipa kiasi cha Sh250 milioni ili kuipata saini ya mfungaji huyo bora wa Ligi Kuu ya Nigeria.

Anas aliyezaliwa Aprili 9, 1998, alikuwa ni mfungaji bora wa Ligi Kuu ya Nigeria (NPFL) kwa msimu wa 2024-2025, baada ya kufunga mabao 18, akihitajika ili kuchukua nafasi ya Mkongomani Heritier Makambo anayetajwa kukaribia kutua Namungo.

Mmoja wa watu wa karibu na mchezaji huyo, aliliambia Mwanaspoti uongozi wa Tabora umepewa wiki hii kuhakikisha dili lake linakamilika kwa kutoa kiasi cha Sh250 milioni, ila tofauti na hapo atafanya biashara na timu nyingine zinazomhitaji.

“Kwa sasa mchezaji yupo Tanzania na amekuja kwa ajili ya kukamilisha uhamisho wake wa kwenda Tabora lakini kwa sharti la kulipa fedha tulizokubaliana, ikishindikana tutaangalia uelekeo mwingine,” alisema mmoja wa watu wanaomsimamia Anas.

Akizungumzia dili hilo, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Tabora United, Mkenya Charles Obiny, alisema wanaendelea na taratibu za kuboresha kikosi hicho kwa ajili ya msimu ujao, japo hawezi kueleza ni mchezaji gani wanayemhitaji hadi watakapomsajili.

“Tetesi ni nyingi kwa sasa hivi kwa sababu ndiyo kipindi chake, nafikiri muda ukifika tutaweka wazi wachezaji wote ambao tutaachana nao na wapya tutakaowasajili, niwaombe tu mashabiki zetu wawe na subra katika kipindi hiki,” alisema Obiny.

Anas mbali na kuichezea Nasarawa United ila ameichezea pia Wikki Tourists zote za kwao Nigeria, akiwa na uwezo mkubwa wa kucheza winga ya kulia na kushoto, huku akiiwezesha Nasarawa kumaliza msimu wa 2024-2025, ikiwa nafasi ya 12 na pointi 52.

Tuzo kwa Anas, imemfanya kushika nafasi ya pili kwa wachezaji wa Nasarawa United, baada ya aliyekuwa nyota wa timu hiyo, Sunusi Ibrahim kuibuka pia mfungaji bora mwaka 2019, baada ya kufunga mabao 10 katika mechi 22 alizochezea kikosi hicho.