Mfanyabiashara auawa kwa risasi Kinondoni

Dar/Tabora. Mfanyabiashara mwenye asili ya Uturuki, Alptekin Aksoy (52) ameuawa kwa kupigwa risasi na watu wasiojulikana waliokuwa wakitumia pikipiki.

Tukio hilo limetokea leo Julai 18, 2025 saa 5:30 asubuhi katika eneo la Kinondoni Makaburini, jijini Dar es Salaam.

Shuhuda wa tukio hilo lililothibitishwa na Jeshi la Polisi, ambaye hakutaka kutaja jina amelieleza Mwananchi kuwa alimuona mtu akishuka kwenye gari lakini ghafla walitokea watu wawili na kumpiga risasi.

“Nilimuona yule baba akishuka kwenye gari alitembea hatua chache ndipo walitokea watu wawili wakiwa kwenye pikipiki wakampiga rirasi mara mbili na wao kukimbia,” amesema shuhuda huyo.

Amesema pamoja na watu wengine walisogea eneo la tukio kuangalia kilichotokea kwani watu hao hawakuchukua chochote zaidi ya kumfyatulia risasi.

Shuhuda mwingine ambaye ni mchuuzi wa matunda eneo hilo amesema hawajui sababu ya mtu huyo kufyatuliwa risasi na ni ngumu kusema kwamba walikuwa majambazi.

“Hatuwezi kusema ni majambazi kwa sababu hawajachukua chochote, baada ya kufanya hivyo tuliposogea tuliona umuhimu wa kutoa taarifa polisi,” amesema.

Baadhi ya vijana wanaoshinda kwenye eneo la makaburi waliozungumza na Mwananchi wamesema walisikia mlio wa risasi, hivyo walielekea eneo la tukio kuona kinachoendelea.

“Tulikuwa tumekaa hapa tukasikia mlio wa risasi mara mbili kama unavyofahamu wananchi hatuna dogo tulivyosikia mlio tukajua kitu kimelipuka lakini tukasikia mara ya pili ikabidi tukimbilie,” amesema mmoja wapo wa vijana hao.

Katika eneo la tukio mwananchi ilishuhudia kukiwa na polisi na baadhi ya watu, huku kukiwa kumefungwa utepe katika Mtaa wa Tunisia.

Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro kupitia taarifa kwa vyombo vya habari amesema wahalifu hao hawakuchukua kitu chochote baada ya kutekeleza tukio hilo.

“Alptekin, raia wa Tanzania mwenye asili ya Uturuki, alishuka kwenye gari lake na kabla ya kuingia ofisini kwake, alivamiwa na kushambuliwa kwa risasi hali iliyosababisha kifo chake papo hapo,” amesema.

Amesema Jeshi la Polisi limeanza uchunguzi wa kina kuhusu tukio hilo.

Kamanda Muliro ametoa onyo kali kwa wote waliohusika, kwamba watakamatwa na kufikishwa kwenye mkono wa sheria kwa hatua zaidi.

Wakati huohuo, mkazi wa Kijiji cha Shitage, wilayani Uyui mkoani Tabora, Zainabu Ndeko (65) amelazwa katika Hospitali ya Manispaa ya Kahama mkoani Shinyanga, baada ya kushambuliwa na watu wasiojulikana.

Ndeko amejeruhiwa maeneo mbalimbali ya mwili wake katika shambulio hilo linalodaiwa kufanywa kwa kutumia silaha yenye ncha kali.

Vyombo vya usalama vinaendelea na uchunguzi ili kubaini wahusika na sababu ya shambulio hilo.

Akizungumza na Mwananchi leo Julai 18, 2025, Josephina Mihayo ambaye ni wifi wa Zainabu, amesema alishambuliwa na watu wasiojulikana usiku wa kuamkia Julai 16, 2025, saa mbili usiku.

Amesema baada ya tukio alipelekwa katika zahanati ya Kijiji cha Shitage alikopewa rufaa kwenda Hospitali ya Manispaa ya Kahama kwa matibabu zaidi.

“Nilipigiwa simu na majirani wa wifi, kwamba amekatwa mapanga mida ya saa mbili usiku, wakampeleka Zahanati ya Shitage, muda mfupi tu wakanipigia tena wameambiwa aje huku Kahama, ndipo nikaenda nikamleta hapa, ni tukio baya kabisa,” amesema.

Mwanaidi Mauba, tabibu katika wodi namba tatu ya Hospitali ya Manispaa ya Kahama, ambako Zainabu amelazwa amesema walimpokea usiku wa kuamkia Julai 16, saa tatu usiku, akiwa katika hali mbaya na mwenye majeraha makubwa.

Amesema walimuanzishia matibabu ya haraka na hali yake inaendelea vizuri, lakini mkono wake wa kushoto ulikatwa kabisa.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, Richard Abwao alipoulizwa na Mwananchi kuhusu tukio hilo, amesema taarifa hazijafika ofisini kwake.

Hata hivyo amesema anaendelea kuzifuatilia na kuahidi kutoa ufafanuzi zaidi baadaye.

“Tukio hilo bado halijaja ofisini kwangu labda nilifuatilie, halafu nitalitolea taarifa baadaye,” amesema.