Arusha. Hofu imetanda jijini Arusha baada ya miili ya wasichana wawili kuokotwa, chanzo cha vifo vyao kikidaiwa ni kubakwa, kulawitiwa, kuvunjwa shingo na kutobolewa macho.
Kutokana na matukio mawili tofauti yenye kufanana, wananchi wameiomba Serikali kupitia Jeshi la Polisi lifanye msako ili kuwabaini watuhumiwa, kuwachukulia hatua kali za kisheria, pia kuimarisha ulinzi na usalama katika maeneo yao.
Katika tukio la kwanza, msichana aliyetambuliwa kuwa Aisha Charles Urio (17), mkazi wa ‘Sokon one’ amekutwa ameuawa na mwili kutelekezwa kwenye nyumba mbovu katika Kata ya Daraja Mbili.
Inaelezwa mwili huo ulikuwa na michubuko kuashiria amebakwa na kulawitiwa, huku shingo na mkono vikivunjwa.
Katika tukio la pili, mwili wa msichana anayekadiriwa kuwa na miaka kati ya 22 na 25 umekutwa kando mwa barabara katika Mtaa wa Kambi ya Fisi, jijini Arusha shingo ikiwa imevunjwa, kutobolewa macho, huku ikielezwa alibakwa na kulawitiwa.
Akizungumzia matukio hayo leo Julai 18, 2025 Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Justine Masejo amesema: “Upelelezi ndio kwanza umeanza, siwezi kusema chochote kwa sasa hadi tutakapobaini chanzo halisi cha matukio hayo au kukamata wahusika.” Amesema miili imehifadhiwa katika Hospitali ya Rufaa Mount Meru kwa taratibu za kiuchunguzi na ukikamilika familia zitakabidhiwa kwa ajili ya maziko.
Kuhusu tukio la kwanza, Zuwena Shabani amesema Aisha alikutwa na kadhia hiyo akiwa katika harakati za kutaka kusafiri kwenda kwa mama yake mzazi baada ya kufukuzwa na mama yake wa kambo.
“Tangu juzi Aisha alikuwa anaaga majirani anasema ananyanyasika na ametakiwa kuondoka, hivyo amewasiliana na mama yake anayeishi Singida na ataondoka kesho yake, siku ya Jumatatu,” amesema na kuongeza:
“Jumatatu asubuhi saa 12 watu wanasema walimuona Aisha na begi kubwa akisafiri, lakini bahati mbaya ndio Jumatano tunapata taarifa kuna mwili wa msichana umeokotwa huko Daraja Mbili kwenye moja ya nyumba mbovu, walivyokwenda kuthibitisha walikuta ni yeye,” amesema.
Zuwena ambaye ni jirani na Aisha amesema inadaiwa alionekana Jumatatu mchana akipata chakula na kuzunguka huku na kule akiwa na kijana anayejihusisha na upigaji debe stendi ya mabasi ya mikoani.
“Baada ya kutokea tukio hilo, kijana anayedaiwa alikuwa naye hakuonekana tena hapa mtaani, wala stendi anakofanya kazi,” amedai.
Mwenyekiti wa Mtaa wa Long’dong, Kata ya Sokon One, Amosi Mndolwa amesema mwili wa Aisha uliokotwa Julai 15, 2025 katika jumba bovu ukiwa na majeraha, kuvunjwa shingo na mkono wa kulia.
“Tulipigiwa simu kuna mwili wa mtu anayesadikiwa kuwa ni wa mtaani kwangu, tulifika eneo la tukio na baadhi ya watu walimtambua ni binti wa mtaani kwetu,” amesema.
Tukio la pili katika Mtaa wa Kambi ya Fisi lililotokea Julai 15, 2025 mwili wa msichana ulikutwa ukiwa uchi ikielezwa alibakwa na kulawitiwa.
Mwenyekiti wa Mtaa wa Kambi ya Fisi, Emanuel Oraya amesema alipigiwa simu alfajiri na wananchi akaelezwa kuna mwili umekutwa barabarani.
“Saa kumi na moja kasoro alfajiri nilipigiwa simu, nilifika kweli nikakuta mwili wa binti huyo uliolazwa kifudifudi ukiwa uchi na alivunjwa shingo na kutobolewa macho, huku akiwa amebakwa na kulawitiwa,” amesema.
Kiongozi huyo wa mtaa amesema: “Nilipiga simu polisi wakaja kuchukua mwili wa marehemu na hadi sasa bado tunasikilizia ni mkazi wa wapi, maana hajafahamika hapa mtaani.”
Ametoa wito kwa wananchi wa Arusha kujitokeza katika Hospitali ya Rufaa ya Mount Meru kuutambua mwili huo.
Mkazi wa mtaa huo, Neema Joram amesema: “Hali hii inatia hofu hasa sisi wajasiriamali ambao kuna muda unachelewa kutoka sokoni kwenye mihangaiko unakutana na balaa kama hili.”
“Arusha inatisha kwa sasa tunaomba polisi waone umuhimu wa kuwasaka watu hawa, wakamatwe na wachukuliwe hatua za kisheria,” amesema.