Watu watatu wafariki dunia, sita wakijeruhiwa katika ajali Iringa

Kilolo. Watu watatu wamepoteza maisha na wengine sita kujeruhiwa baada ya basi dogo kuligonga lori kwa nyuma lililokuwa limesimama katika barabara kuu ya Morogoro-Iringa, eneo la Kijiji cha Imalutwa, Kata ya Lugalo.


‎Akizungumzia ajali hiyo leo Julai 18, 2025 Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, Allan Bukumbi amethibitisha kutokea kwa ajali hiyo kuwa basi hilo aina ya Fuso lililokuwa linaendeshwa na Akhan Mpagile (45), mkazi wa Njombe, liligonga kwa nyuma lori aina ya Howo ambalo lilikuwa limebeba unga kutoka Dar es Salaam.

‎”Dereva wa Fuso, ambaye pia ni miongoni mwa waliopoteza maisha, alifariki papo hapo pamoja na utingo wake Alfred Mgaya na abiria Feleschina Masigati (36) mkazi wa Imalutwa,” imeeleza taarifa ya Kamanda Bukumbi


‎Amesema miili ya marehemu imehifadhiwa katika Hospitali ya Itunda iliyopo Wilayani Kilolo na majeruhi wamepelekwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Iringa.


Taarifa za polisi zinaeleza kuwa dereva wa lori alitoweka eneo la tukio punde baada ya ajali kutokea ambayo chanzo chake ni uzembe wa dereva wa Fuso alishindwa kulimudu gari lake.