Mbeya. Jeshi la Polisi kupitia Kitengo cha Usalama Barabarani mkoani Mbeya limezifungia leseni 42 za madereva, wakiwemo madereva wa masafa marefu, baada ya kubainika kukiuka sheria na kanuni za usalama barabarani kwa kuendesha kwa mwendo hatarishi.
Hatua hiyo imechukuliwa kama sehemu ya mkakati wa kupambana na ajali za mara kwa mara, kwa kutumia mfumo wa Ufuatiliaji wa Mwenendo wa Magari (Vehicle Tracking System – VTS), katika maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Mbeya.
Akizungumza leo Ijumaa, Julai 18, 2025, wakati wa mpango maalumu la ukaguzi wa mabasi ya abiria katika Kituo Kikuu cha Mabasi ya Mikoani, Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani Mkoa wa Mbeya (RTO), Mrakibu Mwandamizi wa Polisi, Notka Kilewa, amesema kuwa leseni hizo zimefungiwa kwa kipindi cha miezi mitatu, huku uchunguzi na ufuatiliaji ukiendelea ili kudhibiti ukiukwaji wa sheria za barabarani.
Ukaguzi huo uliongozwa na Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani nchini, Naibu Kamishna wa Polisi, Fraisser Kashai kutoka Kamisheni ya Mafunzo, ukiwa na lengo la kuhakikisha magari ya abiria yanazingatia vigezo vyote vya usalama kabla ya kuanza safari.
SSP Kilewa aliongeza kuwa katika kipindi cha Januari hadi Juni mwaka huu, jumla ya madereva 42 wamefungiwa leseni kutokana na makosa mbalimbali ya kihatarishi.
Miongoni mwa makosa hayo ni pamoja na kuendesha kwa mwendo kasi, kuyapita magari mengine katika maeneo yasiyoruhusiwa, pamoja na ulevi wakati wa kuendesha magari.
Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani Mkoa wa Mbeya (RTO), Mrakibu Mwandamizi wa Polisi, Notka Kilewa amesema leo Ijumaa Julai 18,2025 wakati wa zoezi la ukaguzi maalumu wa mabasi ya abiria kabla ya kuanza safari.
Ukaguzi huo umefanyika katika kituo kikuu cha mabasi ya mikoani na kuongozwa na Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani nchini na Naibu Kamishna wa Polisi, Fraisser Kashai kutoka Kamisheni ya Mafunzo.
Kilewa amesema wataendelea kuwachukulia hatua za kisheria madereva wanaokiuka sheria sambamba na kuwafungia leseni kwa kipindi cha miezi mitatu, lakini kwa kipindi cha Januari hadi Juni, mwaka huu madereva 42 wamefungiwa leseni.
Ametaja baadhi ya makosa hatarishi yaliyopelekea kufungiwa leseni ni pamoja na mwendo kasi, kuyapita magari mengine katika maeneo yasiyoruhusiwa, ulevi wa pombe wawapo safarini.
“Tutaendelea kukabiliana nao na kuwachukulia hatua, lakini tuwatake kutoa madereva kutoa taarifa za wamiliki wenye mabasi mabovu au dosari ili waweze kufuatiliwa na kuwachukulia hatua kwa kutambua wao ndio wanaopata shida na wawapo barabarani,” amesema.
Katika hatua nyingine, Kilewa ameonya madereva kuhepuka tabia za ulevi kukimbizana wawapo safarini ili kudhibiti ajali za barabarani zisizo za lazima na kulinda maisha ya abiria na mali zao.
Awali akizungumza baada ya kufanya ukaguzi wa mabasi DCP Kashai ametoa tahadhari kwa madereva kuheshimu na kutii sheria ili kuhepuka ajali zisizo za lazima.
Pia, ameisisitiza madereva kutii sheria kwani watakao kiuka na kubainika watachukuliwa hatua za kisheria sambamba na kufungiwa leseni.
Miongozi wa ukaguzi uliofanywa ni pamoja na mabasi ya abiria, leseni za madereva, kupima kilevi sambamba na utoaji elimu ya usalama barabarani kwa abiria lengo kufanya ufuatiliaji na utekelezaji wa maagizo ya Serikali.
Ofisa Mfawidhi wa Mamlaka ya Udhibiti Usafiri wa Ardhini (Latra) Mkoa wa Mbeya, Shaban Mdende amesema katika kukabiliana na ajali za barabarani mabasi ya abiria yamefungwa kifaa maalum cha kudhibiti mwendo.
“Latra tunashirikiana na Polisi usalama barabarani kufanya ufuatiliaji wa mwenendo wa mabasi kwa kutumia kifaa maalumu cha VTS , ambapo kwa kipindi cha Januari hadi Juni kati ya madereva 42 waliofungiwa leseni 26 ni walibainika kupitia mfumo huo,” amesema.
Mkazi wa eneo la Kabwe jijini hapa, Johnson Elius amesema licha ya jitihada za Jeshi la Polisi na Latra kukabiliana na uzembe wa madereva kukiuka sheria bado, kuna maeneo wamekuwa wakishindana kwa kuendesha mwendo kasi.
“Tuishauri Serikali katika kukabiliana na ajali nyingi za barabarani iongeze nguvu ya kufunga mifumo ya kamera maeneo hatarishi ambayo hayana askari wa usalama barabarani jambo ambalo litaleta tija kubwa na kukomesha madereva wazembe,” amesema.