Wanafunzi wawili, bodaboda wafariki kwa ajili Morogoro

Morogoro. Wanafunzi wawili wa kidato cha nne shule ya sekondari Morogoro na dereva wa bodaboda waliyokuwa wamepanda wamefariki dunia papo hapo baada ya pikipiki yao kugongana uso kwa uso na lori la mizigo eneo la Kihonda bima barabara ya Morogoro -Dodoma.

Kwa mujibu wa kamanda wa polisi mkoa wa Morogoro, Alex Mkama amewataja wanafunzi waliofariki kuwa ni Lusajo Benedict mkazi wa Mkomola na Ghalbu Omary mkazi wa Kihonda Maghorifani Manispaa ya Morogoro.

Aidha Kamanda Mkama amemtaja dereva wa bodaboda ambaye naye amefariki dunia ni Baraka Sajio mkazi wa Kihonda Maghorifani na kwamba miili yote ya marehemu hao imehifadhiwa katika hospitali ya rufaa mkoa wa Morogoro.

Akieleza namna ajali hiyo ilivyotokea kamanda Mkama amesema ni baada ya dereva wa bodaboda kutaka kuyapita magari mengine ambapo ghafla aligongana na lori hilo likitokea Dar es Salaam kuelekea Dodoma.

Kamanda Mkama amesema chanzo cha ajali hiyo ni uzembe wa dereva wa bodaboda (marehemu) kutaka kuyapita magari mengine bila ya kuchukua tahadhari.

Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Morogoro, Dk Daniel Nkungu amethibitisha kupokelewa Kwa miili mitatu ambayo ni ya wanafunzi wawili wa shule ya sekondari Morogoro pamoja na bodaboda.

“Ni kweli leo asubuhi tumepokea miili mitatu ya marehemu wakiwemo wanafunzi hao, tumeihidhi miili yote na tayari imeshatambuliwa na ndugu naamini taratibu nyingine za ndugu kuchukua miili ya wapendwa wao zitakuwa zinaendelea,” amesema Dk Nkungu.

Baadhi ya mashuhuda wa ajali hiyo wamesema dereva wa bodaboda hiyo iliyosababisha ajali alikuwa akiendesha Kwa kasi na alikuwa akiyapita magari bila kuchukua tahadhari.

Mmoja wa mashuhuda hao, James William amesema dereva huyo wa bodaboda ambaye kwa sasa ni marehemu bila ya kujali kwamba amepakia wanafunzi wawili (mishkaki) alikuwa akiendesha kwa fujo.

“Mimi nilikuwa kwenye daladala na huyu bodaboda alitupita pale viwandani akiwa kwenye mwendo wa kasi hatukufika mbali tukakuta tayari ameshavamia lori la mizigo na wote walikuwa wameanguka chini wakiwa na hali mbaya kwa kuwa walikuwa na majeraha makubwa na damu zilikuwa zikiwatoka kichwani,” amesema William.

Amesema eneo hilo la Kihonda bima limekuwa na matukio mengi ya ajali lakini wapo baadhi ya madereva hasa wa bodaboda wamekuwa hawajali Wala kuchukua tahadhari wanapofika katika eneo hilo.

Amina Juma ambaye ni mwanafunzi wa shule ya sekondari Morogoro amesema wanafunzi wenzake hao waliacha kupanda daladala na kuamua kupanda bodaboda ili waweze kuwahi mitihani ya wiki.