KILA mwaka Julai 18 dunia huadhimisha Siku ya Kimataifa ya Nelson Mandela kwa kutenga angalau dakika 67 kufanya huduma ya kijamii, kama njia ya kumuenzi shujaa huyo wa Afrika Kusini aliyejitolea maisha yake kupigania haki za binadamu, amani, usawa na utu wa mwanadamu.
Katika kuadhimisha siku hii muhimu mwaka huu 2025, Umoja wa Mataifa nchini Tanzania kwa kushirikiana na Ubalozi wa Afrika Kusini waliungana kwa dakika 67 za huduma ya kijamii katika Makao ya Watoto wenye mahitaji maalumu kilichopo Kurasini, jijini Dar es Salaam.
Tukio hilo limewakutanisha watumishi wa Umoja wa Mataifa, wawakilishi wa kidiplomasia, wadau wa maendeleo, na wanachama wa Jukwaa la Biashara kati ya Afrika Kusini na Tanzania.
Washiriki walijihusisha na shughuli mbalimbali za kijamii zikiwemo kusafisha mazingira, kupanda mimea ya bustani na kusaidia kazi za jikoni, kama ishara ya mshikamano na moyo wa kujitolea aliouacha Mandela.
Jukwaa la Biashara la Afrika Kusini na Tanzania pia walichangia vifaa muhimu kwa ajili ya makao ya watoto wenye mahitaji Maalumu, hatua iliyodhihirisha mshikamano wa sekta binafsi na taasisi za kimataifa katika kusaidia jamii.
Akizungumza wakati wa tukio hilo, Mratibu Mkazi wa Umoja wa Mataifa nchini Tanzania, Susan Namondo amesema;
“Leo tunamuenzi Madiba si kwa maneno bali kwa vitendo. Kila tendo la huduma—hata liwe dogo vipi, huchangia katika kujenga utu, heshima na matumaini. Ushirikiano wetu wa leo ni ushahidi wa nguvu ya umoja na mshikamano.”
Siku ya Nelson Mandela ni wito kwa kila mtu duniani kuleta mabadiliko chanya katika maisha ya wengine. Kauli mbiu ya Mandela “It is in your hands” inakumbusha kuwa kila mtu anao uwezo wa kuleta mabadiliko, hasa kwa wale walio katika mazingira magumu.
“Kwa pamoja, Umoja wa Mataifa Tanzania, Ubalozi wa Afrika Kusini, na wadau wengine wamesimama kwa moyo mmoja kuendeleza urithi wa Mandela kupitia huduma, mshikamano na matumaini.” Amesema