……………
Shirika lisilo la kiserikali la Foundation for Disabilities Hope (FDH) limemkabidhi Kamishna wa Uhifadhi wa Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), CPA(T) Musa Nassoro Kuji tuzo maalumu ya heshima yenye lengo la kutambua mchango mkubwa wa Shirika hilo katika kukuza huduma jumuishi kwa makundi maalum nchini.
Hafla hiyo ya utoaji wa tuzo uliofanyika leo Julai 18, 2025 katika ukumbi wa Mikutano wa TANAPA uliopo jijini Arusha umehudhuriwa pia na Makamishna Waandamizi akiwemo Naibu Kamishna wa Uhifadhi – Massana Mwishawa, maafisa na askari pamoja na wawakilishi waandamizi wa Shirika la Faoundation for Disiabilities Hope
Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa FDH Maiko Salali alieleza kuwa TANAPA imekuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha watu wenye ulemavu hawabaki nyuma katika kunufaika na vivutio vya utalii na huduma jumuishi zinazopatikana ndani ya Hifadhi za Taifa nchini.
Alisema, “Upendo wenu umefanya mabadiliko chanya na umechipua mizizi ya mafanikio yaliyojengwa sanjari na nia yenu njema kwa watu wenye ulemavu”.
Aidha, . Salali aliongeza, “Tunatambua na kuthamini sana mchango wa TANAPA kwa watu wenye ulemavu kwani umechangia na kuinua uchumi kupitia fursa mbalimbali ambazo zimeendelea kutolewa na TANAPA”.
Vilevile, Mkurugenzi huyo alisisitiza, “TANAPA ni shirika la mfano wa kuigwa kwa kufanya huduma zake kuwa jumuishi, tunapokuja TANAPA tunajisikia tuko nyumbani. Maono ya Rais Dkt. Samia katika kusaidia watu wenye ulemavu mnayaendeleza kwa vitendo.”
Kwa upande wake Kamishna wa Uhifadhi – TANAPA CPA (T) Musa Nassoro Kuji alisema, “Kuweka mazingira rafiki na jumuishi kwa watu wote ndiyo dhamira kuu ya TANAPA na tutaendelea kufanya hivyo kwa mustakabali wa Taifa letu.”
Aidha, hivi karibuni Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania lilipewa tuzo yenye mrengo huo kwa kutambuliwa katika mchango wa watu wenye ulemavu kupitia Hifadhi za Taifa Gombe na Mahale katika maonesho ya utalii yaliyofanyika Kigoma mjini. Tuzo iliyokabidhiwa kwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassimu Majaliwa.”