Simba SC yamfuata straika Cameroon

KUNA mazungumzo yanafanyika baina ya viongozi wa Simba na mshambuliaji wa klabu maarufu ya Coton Sport FC de Garoua tayari kuvaa uzi mwekundu msimu ujao.

Mwanaspoti limepata taarifa kutoka chanzo cha ndani cha klabu hiyo, kuhusu uwepo wa mazungumzo ya John Bosco Nchindo (umri 23) wa Cameroon, ambaye kwa mara ya mwisho kucheza mechi mbili za Ligi ya Mabingwa Afrika(CAF) ilikuwa msimu wa 2020/21.

Kama usajili wake utakamilika atakuja kusaidiana na Jean Charles Ahoua kinara wa mabao 16 Ligi Kuu Bara msimu uliyoisha pia alikuwa na asisti tisa, mchezaji mwingine katika nafasi hiyo alikuwepo Awesu Awesu aliyemaliza na mabao mawili, Asisti moja na kapewa mkono kwa bai.

“Kocha Fadlu Davids anatamani kila nafasi iwe na ushindani wa juu, ndiyo maana viongozi wa Simba wapo kazini kutafuta mastaa wa viwango vikubwa, wapo ambao usajili umekamilika na wengine kutofikia mwafaka na wale ambao wanaendelea kuzungumza nao,” kilisema chanzo hicho na kuongeza;

“Kitendo cha Simba kukosa mataji ya Ligi Kuu kwa misimu minne kwa mfululizo kinawanyima raha mashabiki na kujiona wanyonge, ndiyo maana msimu ujao tunahitaji kurejea kwa kishindo.”