Mahariri Mkuu wa Mtandao wa Kijamii wa Torch Media, Caren-Tausi Mbowe ameibuka mshindi wa kwanza katika Tuzo za Uandishi wa Habari za Afya juu ya Udhibiti wa Bidhaa za Tiba zinazotolewa Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba Tanzania (TMDA).
Caren-Tausi ambaye kwa sasa ni Mhariri wa Mtandaoni katika Kampuni ya Sahara Media inayoendesha Televisioni ya Star TV na Radio Free Africa na Kiss FM na Mjumbe wa Kamati Tendaji ya Jukwaa la Wahariri (TEF), ameibuka kidedea na kwa upande wa Majukwaa ya Mtandaoni.
Tuzo hizo zimetolewa wiki hii Julai 16,2025 mkoani Tabora katika hafla fupi baada ya kikao kazi cha kila mwaka baina ya Wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari kutoka jijini Dar es Salaam na wale wa Kanda ya Magharibi inayohusisha mikoa ya Tabora na Kigoma pamoja na Mamlaka hiyo.
Washindi wengine ni Penina Malundo upande wa magazeti (Majira), Julieth mwandishi wa Radio Maria aliyeshinda kwa upande wa Radio na Rehema Evance wa Azam Media aliyeibuka mshindi kwa upande wa Television.
Akikabidhi Tuzo hizo ,Mkurugenzi Mkuu, Dk Adam Fimbo alisema jumla ya waandishi 28 waliowasilisha kazi zao.
Dk Fimbo alisema Tuzo hizo zilianza mwaka 2021 na tangu wakati huo zimekuwa zikifanyika kila mwaka na kuwataka waandishi kujitokeza kwingi ili kuongeza wigo wa habari za Afya kwa upande wa Udhibiti wa Dawa na Tiba.
Akizungumza mara baada ya kupokea Tuzo hiyo iliyoambatana na zawadi ya fedha taslimu, Caren-Tausi aliwataka waandishi wa Habari kupenda kuandika habari za Afya ili kuelikisha jamii.
” Leo ninafura kubwa pamoja na kwamba nimeshinda lkn nimeweza kuifikia jamii kupitia kalamu yangu kwa kuwaelimisha. Niwaombe waandishi wenzangu hasa wahariri tusiache.kuandika kwa sababu nasi ni waandishi pia.”
