Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Amos Makalla, amesema maandalizi ya mchakato wa uchaguzi ndani ya chama hicho yanaendelea kwa umakini mkubwa, huku akithibitisha kuwa kikao cha mwisho cha uteuzi wa wagombea wa nafasi za Ubunge na Udiwani kupitia kura za maoni kimepangwa kufanyika Julai 28, 2025.
Makalla ametoa taarifa hiyo leo akiwa jijini Dodoma, akieleza kuwa awali Kamati Kuu ya chama hicho ilipangwa kuketi leo Julai 19 kwa ajili ya kufanya uteuzi wa mwisho, lakini kikao hicho kimeahirishwa hadi Julai 28 kutokana na wingi wa majina ya watia nia na hitaji la kuyachambua kwa uangalifu ili kuhakikisha haki inatendeka.
“Maandalizi ya mchakato wa uchaguzi ndani ya CCM yanaendelea vizuri. Kamati Kuu ya Chama ambacho ilikuwa iketi leo kwa ajili ya kufanya uteuzi wa mwisho kwa wagombea wa nafasi za Ubunge na Udiwani, sasa itaketi Julai 28 hapa hapa Dodoma,” alisema Makalla.
Ameongeza kuwa kabla ya kikao hicho cha Kamati Kuu, kutafanyika kikao cha Halmashauri Kuu ya CCM Taifa (NEC) mnamo Julai 26, 2025, ikiwa ni sehemu ya taratibu za ndani za chama katika kupitisha majina ya wagombea.
Makalla pia amewatoa hofu watia nia waliokuwa wakisubiri maamuzi ya leo, akiwataka kuwa watulivu huku mchakato ukiendelea kwa umakini ili kuhakikisha kila hatua inazingatia haki na usawa.
“Wagombea sasa watulie, wajue mchakato unaendelea kwa makini. Unajua watia nia ni wengi sana, kwa hiyo kazi ya kuchambua ni kubwa na sisi tunataka tutende haki. Sasa wapumzike tu mpaka tarehe 28 ambapo uteuzi wa mwisho utafanyika,” alisisitiza.
Makalla alihitimisha kwa kueleza kuwa kumekuwa na mawasiliano mengi ya simu kutoka kwa watu waliotaka kufahamu hatma ya vikao hivyo, hivyo taarifa aliyoitoa leo ndiyo rasmi kutoka ndani ya chama.
“Nimepokea simu nyingi sana watu wakitaka kujua hatma ya kikao, lakini sasa naomba watulie, hiyo ndiyo taarifa rasmi ya chama,” alisema.
Mchakato huu ni sehemu ya maandalizi ya CCM kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Serikali za Mitaa na Uchaguzi Mkuu wa 2025, ambapo chama hicho kimeweka mkazo mkubwa kwenye uwazi, haki na umakini katika kupitisha wagombea wake.