UONGOZI wa Singida Black Stars umefikia makubaliano ya kuachana na kiraka, Edward Charles Manyama baada ya kuitumikia kwa msimu mmoja.
Manyama alijiunga na Singida BS msimu uliomalizika kwa mkataba wa miaka miwili akiwa mchezaji huru baada ya kumaliza mkataba wake na Azam FC.
Chanzo cha kuaminika kutoka ndani ya Singida Black Stars kimeliambia Mwanaspoti kuwa uongozi wa timu umefikia makubaliano na nyota huyo ili kupisha usajili mwingine.
“Ni kweli tumefanya mazungumzo na mchezaji huyo na kufikia makubaliano ya kuvunja mkataba wa mwaka mmoja uliokuwa umebaki ili kupisha usajili wa nyota wengine na kumpa nafasi ya kutafuta changamoto nyingine katika dirisha hili,” alisema mtoa taarifa huyo na kuongeza;
“Tunathamini mchango wake kwenye kikosi chetu akiitumikia Singida kwa msimu mmoja sasa tunapambana kuimarisha kikosi ambacho tunatarajia kitakuwa na ushindani ndani na kimataifa baada ya kupata nafasi ya uwakilishi.”
Mbali na Manyama pia Singida imeachana na Habib Kyombo na winga Hamad Majimengi ambao wote walikuwa kwa mkopo nje ya timu hiyo baada ya kumaliza mikopo yao wamefanya mazungumzo ya kumalizana nao.
Mwanaspoti lilimtafuta Ofisa Habari wa Singida Black Stars, Hussein Massanza ambaye alithibitisha kuwa kwenye mazungumzo na wachezaji hao kwa ajili ya kuvunja mikataba huku akiweka wazi kuwa muda ukifika wataweka wazi.
“Ni kweli tupo kwenye mazungumzo na baadhi ya wachezaji wakiwamo hao kwa ajili ya kufikia makubaliano ya pande zote mbili ili kuvunja mikataba na kama tutafanikiwa tutatoa taarifa ni wachezaji gani tutaendelea nao na wangapi tutaachana nao sambamba na kutangaza sajili mpya.”