Pogba wa Zenji, Simba mambo sio freshi

BAADA ya Simba kushindwa kukamilisha mchakato wa kumsajili kiungo wa Mlandege, Juma Kidawa ‘Pogba’, mchezaji huyo yupo katika hatua za mwisho kumalizana na Tabora United.

Simba ilionyesha nia ya kunasa saini ya kiungo huyo aliyecheza mechi zote 30 msimu huu akiwa na Mlandege iliyotwaa ubingwa wa Ligi Kuu Zanzibar (ZPL) na kufikia hatua ya kumtumia tiketi ya ndege lakini mambo hayajafanikiwa.

Akizungumza na Mwanaspoti, Pogba alisema ni kweli alitumiwa tiketi ya ndege na Simba, lakini uongozi wa Mlandege ulimzuia kusafiri kutokana na kuthibitisha kuwa klabu haijapokea fedha kama walivyokubaliana na Wekundu hao.

“Dili la Simba halijaeleweka hadi muda huu licha ya kutumiwa hadi tiketi ya ndege mchakato uliopo sasa ni viongozi kuwa katika mazungumzo na Tabora United ambayo imeonyesha nia ya kunihitaji,” alisema kiungo huyo na kuongeza;

“Wasimamizi wangu wanaendelea na mazungumzo na timu zote mbili lakini asilimia kubwa zipo kwa Tabora United kutokana na kuonyesha uhitaji zaidi hii ni baada kuja hadi Zanzibar tofauti na Simba ambayo ilipiga simu na ukimya unaendelea kutawala.”

Pogba alisema yupo tayari kucheza timu yoyote anachoangalia ni maslahi na matamanio yake ni kucheza Ligi Kuu Bara na anaamini itakuwa sehemu ya yeye kufanikisha mipango yake.

Pogba ni zao la kituo cha michezo cha FTI kilichopo Afrika Kusini na huu ni msimu wake wa pili kuichezea Mlandege akiitumikia katika mechi zote 30.