BAADA ya kukosekana uwanjani msimu uliopita, kipa Mohamed Makaka amesema kwa sasa yupo tayari kukipiga popote, akieleza kuwa uwezo na uzoefu alionao timu yoyote namba ni uhakika.
Makaka aliyewahi kukipiga timu kadhaa ikiwamo Stand United na Gwambina, msimu uliopita alijikuta nje ya uwanja baada ya kuumia goti alipokuwa akikiwasha Mtibwa Sugar aliyoshuka nayo daraja.
Staa huyo ameliambia Mwanaspoti, kwa sasa anaendelea kujifua akisikilizia simu yoyote itakayomwita kwa ajili mazungumzo tayari kwa kurejea upya uwanjani, akieleza kuwa kwa sasa hachagui timu ya kufanyia kazi.
Alisema pamoja na kuwa nje ya uwanja kwa takribani msimu mzima, haiwezi kupunguza ubora wake kwakuwa tangu amerejea mazoezini, anaona afya ikiimarika na timu yoyote anao uhakika wa namba.
“Kwa sasa naendelea na mazoezi binafsi na niko tayari kurejea uwanjani, siwezi kuchagua timu kwa kuwa kazi yangu ni mpira, najivunia uwezo na uzoefu, popote uwezekano wa namba ni uhakika,”€ alisema Makaka.
Kipa huyo, alisema kuwa anapojiweka fiti, anafahamu ugumu wa ligi ulivyo, akibainisha anaamini msimu ujao atafanya makubwa zaidi.