Lugha ya Kiswahili imetambuliwa rasmi kuwa chombo muhimu katika kukuza uelewa wa kisheria na kitamaduni kati ya Tanzania na China, kufuatia uzinduzi wa tafsiri ya kwanza ya maandiko ya kisheria kutoka China kwenda Kiswahili.
Uzinduzi huo umefanyika jijini Dar es Salaam kupitia kongamano lililowakutanisha wataalamu wa tafsiri, wachapishaji na wasomi kutoka mataifa hayo mawili. Viongozi wa taasisi mbalimbali wameipongeza hatua hiyo, wakisisitiza kuwa ni mwanzo mpya wa ushirikiano wenye tija kwa wananchi wa pande zote mbili.
Mkurugenzi wa Taasisi ya Taaluma za Kiswahili (Tataki), Profesa Aldin Mutembei, amesema ufunguzi wa fursa kwa Watanzania, kwa mara ya kwanza Watanzania wataweza kupata maarifa ya sheria za China kupitia lugha wanayoielewa. “Hili ni jambo kubwa, kwani linarahisisha mawasiliano ya kisheria baina ya nchi hizi mbili,” amesema Prof. Mutembei.

Naye Kulwa Kindija kutoka Baraza la Kiswahili la Taifa (Bakita) amesema kuwa hatua hiyo inaunga mkono jitihada za serikali za kukuza matumizi ya Kiswahili katika sekta ya sheria. Amebainisha kuwa istilahi mbalimbali zimeanza kuandaliwa ili kurahisisha tafsiri sahihi ya maandiko ya kisheria.
Kwa upande wake, Husna Sharif kutoka Chama cha Maendeleo ya Urafiki kati ya Tanzania na China, kupunguza migogoro na kukuza maelewano amesema tafsiri hizi zitapunguza migogoro midogo inayotokana na kutokuelewana, hasa katika masuala ya biashara na uhamiaji. “Kwa lugha ya pamoja, kila upande utaelewa haki na wajibu wake kisheria,” amesisitiza.
Akizungumza katika kongamano hilo, Prof. Ao Manyun kutoka Chuo Kikuu cha Mawasiliano cha China amesema Kiswahili ni lugha ya kimataifa inayozidi kupata umuhimu mkubwa, ambapo nchini China kimekuwa kikifundishwa kwa zaidi ya miaka 65 na tayari wahitimu zaidi ya 540 wamejifunza lugha hiyo.
Prof Manyun amefafanua kuwa tafsiri ya maandiko ya kisheria ni hatua muhimu katika kuimarisha mahusiano ya kiutamaduni na kisheria. “Niliona ni vyema kutafsiri vitabu vya sheria kwa Kiswahili ili kuwasaidia raia wa China wanaofanya biashara Tanzania kuelewa sheria za ndani na kuepuka migogoro isiyo ya lazima,” amesema.
Ameongeza kuwa tafsiri ya sheria kama zile zinazohusu haki halisi itawawezesha wageni kuelewa namna ya kumiliki mali au kushiriki miradi ya pamoja kwa mujibu wa taratibu halali.
Hatua hii imeelezwa kuwa ishara ya uhusiano wa kina na wa kimkakati kati ya Tanzania na China, unaojengwa si tu kwa misingi ya kibiashara, bali pia kwa uelewano wa kijamii na kisheria kwa kutumia Kiswahili kama daraja la mawasiliano.