Mradi wa uchimbaji urani kuongeza upatikanaji umeme

Songea. Waziri wa Madini, Anthony Mavunde amesema mradi wa kimkakati wa uchimbaji urani utaanza hivi karibuni baada ya kukamilika ujenzi wa kiwanda cha majaribio cha uchenjuaji wa madini hayo.

Amesema hayo jana Julai 18, 2025 akiwa wilayani Namtumbo, mkoani Ruvuma alikotembelea kukagua maendeleo ya ujenzi wa mradi huo unaokadiriwa kugharimu Sh3.06 trilioni unaotekelezwa na Kampuni ya Mantra Tanzania Limited.

Mavunde amesema moja ya vipaumbele vya Serikali kwenye sekta ya madini ni kuyaongeza thamani ndani ya nchi, jambo linalosimamiwa na wizara yake.


“Kuanza kwa mradi huu ambao unahusisha pia ujenzi wa kiwanda cha kuongeza thamani madini ya urani kunadhihirisha utekelezaji wa azma ya Serikali kwa vitendo. Katika hili, sisi Wizara ya Madini tutaendelea kusimamia kikamilifu ili kunufaisha nchi yetu,” amesema.

Uwepo wa mashapo yanayokadiriwa kufikia tani milioni 139 na kufanya maisha ya mgodi kukadiriwa kuwa miaka 22, kunaifanya Tanzania kuingia kwenye ramani ya dunia na kuwa miongoni mwa nchi 10 zinazozalisha madini ya urani kwa wingi duniani.

Akizungumzia manufaa ya mradi huo, Mavunde amesema ukiachana na ajira za moja kwa moja zaidi ya 4,000 na zisizo za moja kwa moja zaidi ya 100,000, Kampuni ya Mantra imeanza majadiliano na Serikali ili kuhakikisha inajenga mtambo wa kuzalisha umeme kwa kutumia urani itakayochimbwa mgodini hapo.

Tayari Serikali imetangaza kuanza kutekeleza mpango wa ujenzi wa kituo cha kuzalisha umeme wa gesi cha Kinyerezi III, kitakachozalisha megawati 1,000 eneo la Kinyerezi, jijini Dar es Salaam.


Mbali na mradi huo, tayari mashine zote tisa za kuzalisha umeme katika Bwawa la Kufua Umeme wa Maji la Julius Nyerere (JNHPP) zimekamilika na zimeanza kuzalisha jumla ya megawati 2,115. Mashine ya mwisho iliwashwa Aprili 5, 2025, kila moja inazalisha megawati 235.

Mavunde amesema licha ya manufaa makubwa kwa Taifa kupitia mapato, mradi huo unakwenda kubadilisha taswira ya Namtumbo kwani unakwenda kugusa maisha ya wananchi wengi wanaozunguka mradi.

Awali, Meneja wa Uendelezaji Mradi kutoka Kampuni ya Mantra, Majani Moremi aliishukuru Serikali kwa kuendelea kutoa ushirikiano kwa kampuni hiyo uliowezesha uanze kutekelezwa.


Ameahidi mradi unakwenda kuleta tija na mafanikio yanayotarajiwa kwa Taifa.

Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Ahmed Abbas amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuweka mazingira rafiki ya uwekezaji nchini yaliyowezesha mradi huo kutekelezwa mkoani Ruvuma.

Ameahidi kuendelea kutoa ushirikiano kwa Kampuni ya Mantra muda wote ili kufanikisha utekelezaji wa mradi huo kwa manufaa ya nchi na wananchi wa Namtumbo.