Dar es Salaam. Katibu wa Kanisa la Anglikana Tanzania, Mchungaji George Lawi ameikana katiba ya kanisa hilo ambayo ni kielelezo cha ushahidi katika kesi ya mgogoro wa zawadi ya shamba na nyumba alizopewa Askofu mkuu wa kwanza wa kanisa hilo nchini, John Sepeku.
Mchungaji Lawi ameikana katiba hiyo wakati akitoa ushahidi wake katika kesi hiyo, inayosikilizwa na Jaji Arafa Msafiri, kqwenye Mahakama Kuu Divisheni ya Ardhi, akiwa ni shahidi wa pili wa upande wa wadaiwa katika kesi hiyo.
Kesi hiyo imefunguliwa na mtoto wa Askofu Sepeku, Bernado Sepeku, dhidi ya Bodi ya Wadhamini wa Kanisa la Anglikana Tanzania, Askofu wa Dayosisi ya Dar es Salaam, Jackson Sosthenes na kampuni ya Xinrong Plastic Waste Industry Co Ltd.
Bernado alifungua kesi hiyo mwaka 2023 baada ya kubaini kuwa uongozi wa sasa wa dayosisi hiyo chini ya askofu wake, Sosthenes uliligawa shamba hilo ambalo kwa sasa linadaiwa kuwa na thamani ya Sh3.7 bilioni kwa mwekezaji – kampuni ya Xinrong Plastic Waste Industry Co Ltd.
Mwekezaji huyo baada ya kugawiwa shamba hilo ambamo walikuwa wamejenga nyumba mbili, alifyeka mazao mbalimbali waliyokuwa wameyalima, kisha akajenga kiwanda na nyumba yenye thamani ya Sh165 milioni.
Kwa mujibu wa ushahidi wa upande wa madai uliotolewa na mashahidi mbalimbali wakiwemo wajumbe wa bodi ya wadhamini na maaskofu wengine wa kanisa hilo, Askofu Sepeku alipewa zawadi hiyo na Dayosisi ya Dar es Salaam mwaka 1980.
Pendekezo la kumzawadia Askofu Sepeku shamba na nyumba lilitolewa awali na Kamati ya Kudumu ya Kanisa hilo Dayosisi ya Dar es Salaam katika kikao chake cha Desemba 8, 1978.
Sinodi ya Dayosisi hiyo katika kikao chache cha Machi 8 na 9, 1980 iliridhia na kuazimia kumpatia Askofu Sepeku zawadi ya ardhi, shamba la eka 20 lililoko Buza wilayani Temeke, Dar es Salaam na nyumba eneo la Kichwere, Buguruni, wilayani Ilala, Dar es Salaam.
Hata hivyo, Mchungaji Lawi ambaye aliieleza Mahakama kuwa pia ni Katibu wa bodi ya wadhamini wa kanisa hilo nchini (mdaiwa wa kwanza), katika ushahidi wake aliouhitimisha Julai 18, 2025, amekana kutambua shamba na nyumba hiyo kutolewa kwa Askofu Sepeku kama zawadi.
Amekana kuitambua zawadi hizo akiongozwa na wakili wa wadaiwa, Denis Malamba na ushahidi wa nyongeza, akihojiwa maswali ya dodoso na mawakili wa wadai, Deogratius Butawantemi na Gwamaka Sekela.
Mchungaji Lawi amedai kuwa kwa mujibu wa muundo wa kanisa hilo, mmiliki wa mali zote ni Bodi ya Wadhamini na Dayosisi au makanisa moja moja ni waangalizi tu na hivyo wadhamini ndio wana mamlaka ya kufanya lolote kuhusiana na mali hizo.
Amedai kuwa kwa kuwa Bodi ya Wadhamini hazikuwahi kukaa na kuamua kumpa Askofu Sepeku zawadi hizo, nyumba na shamba (maana hakuna kumbukumbu zozote zinazoonyesha hivyo, basi shamba na nyumba hiyo ni mali ya wadhamini kwa kuwa dayosisi si mmiliki wa mali hizo na hivyo haina mamlaka ya kuzigawa.
Hata hivyo, madai yake ni kinyume na katiba ya kanisa hilo ya mwaka 1970 iliyokuwa unatumika wakati Askofu Sepeku anapewa zawadi hizo na Sinodi ya Dayosisi baada ya kuridhika pendekezo la Kamati ya Kudumu ya dyosisi hiyo.
Katiba hiyo ambayo ilipokewa na kusajiliwa kuwa moja ya vielelezo vya ushahidi wa mdai, inazipa nguvu na mamlaka Sinodi za Dayosisi dhidi ya mali zake zilizo chini ya wadhamini wa kanisa hilo.
Katiba hiyo inabainisha kuwa wamiliki wa mali ni dayosisi au makanisa mojamoja ndani ya dayosisi, ambazo ndizo zina mamlaka ya kukubali masharti yoyote kuhusiana na mali hizo huku ikisisitiza kuwa wadhamini ni waangalizi tu.
Alipoelekezwa na Wakili Butawantemi katika katiba hiyo, wakati akimhoji maswali ya dodoso, ndipo Mchungaji Lawi alipoikana, badala yake alieleza kuwa katiba anayoitambua ni ya mwaka 2004 (marekebisho ya katiba ya awali ya mwaka 1970).
Amesema Katiba hiyo ya mwaka 2004 ndio inabainisha utaratibu wa matumizi ya mali hizo na wenye mamlaka kuwa ni wadhamini.
Kifungu cha 21 (c) kama alivyokisoma mahakamani wakili wa mdai, Butawantemi kinaeleza kuwa:
Wadhamini wa Kanisa Anglikana Tanzania watatunza mali yote waliyokabidhiwa au watakayokabidhiwa amana kwa ajili ya jimbo au dayosisi au kanisa lolote la dayosisi.
Ikiwa mali ni ya jimbo, masharti yatakayowekwa juu ya dhamana hayana budi kukubaliwa na Sinodi ya Kanisa Anglikana Tanzania, na ikiwa mali ni ya dayosisi au mojawapo ya makanisa yake, masharti yake hanaya budi kukubaliwa na Sinodi ya Dayosisi.
Hata hivyo, katiba hiyo ambayo Mchungaji Lawi alitaka izingatiwe, ilikataliwa na Mahakama kupokewa kuwa kielelezo cha upande wa utetezi, baada ya kuwekewa pingamizi na mawakili wa mdai na kuwa haikukidhi matakwa ya kisheria kupokewa na kuwa kielelezo.
Sambamba na hilo, ni kanuni ya kisheria kuwa sheria inapofanyiwa marekebisho au inapotungwa mpya, marekebisho hayo au sheria hiyo mpya huanza kutumika kuanzia wakati huo, baada ya marekebisho hayo.
Alipohojiwa na Wakili Butawantemi, amejibu kuwa hajui nani alimweka Sepeku katika nyumba ya Buguruni ambamo familia yake inaishi mpaka sasa na katika shamba la Mtoni Buza ambamo wamejenga nyumba mbili.
Pia, amejibu kuwa hajawahi na wala hana kumbukumbu za kumfungulia Askofu Sepeku/familia yake kesi ya uvamizi wa nyumba na shamba hilo.
Wakati akihojiwa na wakili wake, Malamba akitoa maswali ya kumwongoza kutoa ufafanuzi wa baadhi ya majibu kwa maswali ya mawakili wa wadai, Mchungaji Lawi pamoja na mambo mengine amesisitiza yale aliyoyaeleza katika ushahidi wa msingi.
Amedai kuwa mali hizo zinazodaiwa kutolewa kama zawadi kwa Askofu Sepeku ni mali za Bodi ya Wadhamini na kwamba Sinodi ya Dayosisi ya Dar es Salaam haina nguvu ya kutoa mali kama zawadi, hasa zilizoko kwenye orodha ya mali za wadhamini, kwani haina Bodi ya Wadhamini.
Katika esi hiyo itakayoendelea Agosti mosi, 2025, Bernado ambaye ni msimamizi wa mirathi ya baba Askofu Sepeku anaiomba Mahakama iamuru alipwe Sh3.72bilioni ambayo ni fidia ya hasara ya kifedha iliyopatikana kutokana na uvamizi wa mali ya ardhi katika kiwanja hicho.
Pia, anaiomba alipwe Sh493.65 milioni kama fidia ya hasara ya mazao yaliyoharibiwa katika shamba hilo.
Miongoni mwa mashahidi waliotoa ushahidi upande wa mdai ni pamoja na aliyewahi kuwa Askofu wa Dayosisi ya Dar es Salaam, Dk Valentino Mokiwa, ambaye pamoja na mambo mengine, alieleza kuwa uamuzi wa Sinodi hauwezi kutenguliwa na askofu yeyote.