Hawa ndio waliowalipua polisi kwa mabomu, moja liliharibiwa na JWTZ

Songea. Mahakama ya Rufani Tanzania, imebariki kifungo cha miaka 15 jela, walichohukumiwa wakazi watatu wa mjini Songea, waliowalipua askari wa Jeshi la Polisi kwa mabomu mawili yaliyotengenezwa nyumbani na kujeruhi polisi wanne.

Bomu la tatu lilitegeshwa katika kibanda wanachokitumia Askari wa Usalama Trafiki na waya wake ukaenda meta kadhaa porini kulipokuwa na kilipuzi, lakini hata hivyo bomu hilo liliharibiwa na wataalamu wa Jeshi la Wananchi (JWTZ).

Katika hukumu yao waliyoitoa Julai 11,2025 na kuwekwa mtandaoni Julai 18, 2025 Jopo la majaji watatu wa mahakama ya Rufani, Augustine Mwarija, Rehema Kerefu na Omar Makungu, limebariki adhabu hiyo iliyotolewa Desemba 22,2023.

Ni kutokana na majaji hao kuthibitisha hukumu hiyo iliyotolewa na Jaji Elinaza Luvanda, sasa ni rasmi kuwa Juma Msabila, Hamza Yusuph na Yassin Mussa, ndio waliohusika na mashambulizi hayo ya mabomu dhidi ya Askari wa Jeshi la Polisi.

Katika moja ya mashambulizi hayo, mmoja wa magaidi, Hamis Omary alifariki dunia kutokana na mlipuko uliosababishwa na bomu alililolirusha na simu yake ndio iliyosaidia kukamatwa kwa mrufani wa pili katika kesi hiyo, Hamza Yusuph.

Lengo la mashambulizi hayo yaliyotokea mwaka 2014, ilikuwa ni kuwapora silaha za moto askari polisi, ili Juma, Hamza, Mussa na wengine ambao sio sehemu ya rufaa hiyo, waweze kuipindua Serikali ya Tanzania na kuanzisha Dola ya Kiislamu.

Shitaka la kwanza lilikuwa ni la kula njama ambapo kati ya Januari 1,2014 na Desemba 2014, walikula njama ya kuwashambulia askari polisi kwa mabomu kisha kupora silaha ambazo wangezitumia kutekeleza mashambulizi ili kupindua Serikali.

Kwa mujibu wa hukumu hiyo, shitaka la pili lilikuwa ni la kushiriki mikutano ya kigaidi kwa lengo la kupanga namna ya kutekeleza matukio ya ugaidi ambapo shitaka la tatu ni kukusanya Sh1.6 milioni ili zitumike kwa shughuli ya ugaidi.

Katika kosa la 4 hadi la 8, walishitakiwa kwa kutekeleza vitendo vya kigaidi kwa kuwashambulia polisi kwa mabomu katika maeneo mawili tofauti huku katika tukio la tatu, wataalamu wa JWTZ walifanikiwa kutegua bomu walilolitega.

Jaji Luvanda baada ya kusikiliza ushahidi, aliwatia hatiani washitakiwa hao katika shitaka la kwanza hadi la nane na shitaka la 10 hadi la 14 na kuwahukumu kifungo cha miaka 15 jela kila shitaka na vifungo vyote vingetumikiwa kwa pamoja.

Hata hivyo, hawakuridhishwa na hukumu hiyo na kukata rufaa wakiegemea sababu mbili za rufaa, moja ikiwa ni kuwa mahakama ilikosea kisheria kuwatia hatiani kwa kuegemea vielelezo ambavyo vilikuwa kinyume cha sheria.

Sababu ya pili ni kuwa mahakama ilikosea kisheria na kiushahidi kwa kuwatia hatiani warufani kwa kuegemea ushahidi ambao haukuungwa mkono, ulikuwa wa kujikanganya na ambao haukutosha kuifanya mahakama iwatie hatiani.

Katika rufaa hiyo, mrufani wa kwanza aliwakilishwa na wakili Edson Mbogoro huku wa pili na wa tatu wakiwakilishwa na mawakili Vicent Kassale na Eliseus Ndunguru, huku Jamhuri ikiwakilisha jopo la mawakili saba wa Serikali.

Mawakili hao ni wakili wa Serikali mkuu, Faraja Nchimbi aliyesaidiana na mawakili wa Serikali wakuu, Salim Msemo, Sabrina Joshi na Ofmedy Mayenga na mawakili waandamizi wa Serikali, Valence Mayenga, Faraja George, Ignas Mwinuka na Clara Charwe.

Katika uchambuzi wao, majaji walianza kwa kueleza kuwa mwaka 2014, wakazi wa Manispaa ya Songea katika mkoa wa Ruvuma, walishuhudia matukio matatu ya mashambulizi dhidi ya maofisa wa polisi walikuwa katika doria za kila siku.

Tukio la kwanza lilitokea Septemba 16,2014 katika mtaa wa Maliatabu katika eneo la Mabatini mjini Songea ambapo usiku huo, maofisa watano wa Jeshi la Polisi, wawili kati yao wakiwa na silaha, walikuwa wakifanya doria katika eneo hilo.

Walishambuliwa na watu wawili waliowasogelea kutokea nyuma wakiwa na pikipiki, walipowapita tu kwa haraka, waliwarushia maofisa hao bomu ambalo lililipuka na kuwajeruhi maofisa hao, huku wawili wakipata majeraha.

Tukio la pili lilitokea Oktoba 27,2014 katika eneo la Mshangao pia katika Manispaa ya Songea ambapo kuna kibanda ambacho hutumiwa na askari wa usalama barabarani kupumzikia wanapohitaji kupumzika wanapokagua magari.

Katika eneo hilo kulikuwa na ‘benchi’ ambalo hulitumia kukaa wanapohitaji kupumzika ambapo Ofisa mmoja aliyekuwa shahidi wa 4, alishuku kitu kisicho cha kawaida na baada ya kuchunguza aliona waya umefukiwa ardhini eneo hilo.

Waya huo ulikuwa umeenda hadi msitu uliopo jirani na eneo hilo na baada ya ukaguzi wa kina wa wataalamu kutoka JWTZ, ilibainika kuwa waya huo ulikuwa umeunganishwa na bomu, ambalo wataalamu hao walifanikiwa kulitegua.

Haikuishia hapo, kwani Desemba 25,2014 katika eneo la Majengo Quarters lilitokea tukio lingine ambapo maofisa polisi watano, wawili wakiwa na bunduki, walishambuliwa kwa bomu na watu wawili waliokuwa katika pikipiki.

Mlipuko huo uliwajeruhi maofisa polisi wawili ambao ni shahidi wa 7 na 13 lakini mlipuko huo ulisababisha kifo cha mmoja wa waliorusha bomu hilo.

Kufuatilia matukio hayo, kikosi maalumu cha makachero wa kuchunguza matukio makubwa, yakiwamo ya ugaidi, kutoka ofisi ya Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Jijini Dar es Salaam, kiliingia kazini kuwasaka wahalifu hao.

Ni kutokana na upelelezi huo, walifanikiwa kuwakamata warufani pamoja na watu wengine, ambapo walihojiwa na kuandika maelezo ya kukiri kushiriki makossa hayo na ndipo mwisho wa siku wakatiwa hatiani na kuhukumiwa miaka 15 jela.

Kuhusu hoja za warufani, majaji hao walisema kumbukumbu zinaonyesha baada ya kukamatwa katika maeneo mbalimbali na tarehe tofauti tofauti na kwa maelekezo ya DCI, warufani hao walipelekwa Dar es Salaam kwa ajili ya uchunguzi wa kikosi maalum.

Kulingana na shahidi wa 25, walisafirishwa kwenda Dar es Salaam wakitokea Songea Januari 4,2025 saa 8:00 mchana, ushahidi ambao uliungwa mkono na mashahidi namba 6,17,21 na 26 ambao walikuwa miongoni wa timu hiyo.

Kwa mujibu wa ushahidi wa shahidi wa 26 uliopo katika jalada la rufaa hiyo, walifika Dar es Salaam saa 1:00 asubuhi hivyo majaji wakasema kisheria, mtuhumiwa anatakiwa aandike maelezo yake ndani ya saa 4 tangu akamatwe.

“Kwa kuwa walisafirishwa kwa gari na wakafika asubuhi ya siku inayofuata, maelezo yao yaliandikwa ndani ya muda. Hatuoni mashiko katika hoja ya kwamba maelezo yao hayo yaliandikwa nje ya muda. Hoja hii haina msingi,” walieleza.

“Kulikuwa na hoja kuwa maelezo ya mshitakiwa wa tatu (Yasin) yalionekana hayana uhalali na mahakama lakini yakazingatiwa wakati wa kuwatia hatiani warufani. Huo ni msimamo sahihi,”walieleza majaji hao katika hukumu yao.

Kwa mujibu wa majaji hao, wakati Jamhuri ilipotaka kuyatoa maelezo hayo kama kielelezo cha kesi, upande wa utetezi ulipinga na kuibuka kwa kesi ndani ya kesi baada ya upande wa utetezi kudai kuwa mrufani hakuandika maelezo hayo.

“Baada ya kesi ndani ya kesi, maelezo hayo yalipokelewa lakini hoja ya kisheria iliyoibuliwa na wakili wake kuwa maelezo hayo hayakuthibitishwa, hoja hiyo iliahirishwa kwamba ingeshughulikiwa wakati wa kutoa hukumu,” walisema.

Wakirejea hukumu ya Jaji Luvanda, majaji hao walisema Jaji alikosea kisheria, kimantiki na ushahidi kwa kumtia hatiani mrufani wa tatu kwa kuegemea kielelezo hicho batili.

“Baada ya kuona maelezo hayo hayakusainiwa na mrufani wa tatu ili kuthibitisha maudhui yaliandikwa na yeye, kielelezo hicho hakikustahili kutumiwa na mahakama kumtia hatiani. Hivyo tunakubaliana na wakili Ndunguru,”walieleza.

Kuhusu sababu ya pili, majaji hao walisema upande wa Jamhuri haikuwa umeegemea tu kwenye maelezo ya onyo ya washitakiwa katika kuwatia hatiani, bali iliegemea ushahidi wa mdomo wa mashahidi wengine na vielelezo.

“Hoja iliyoibuka katika rufaa hii ni kama maungamo ya mrufani wa kwanza na wa pili yaliungwa mkono na mashahidi wengine. Mawakili wote wa utetezi walisema hayakuungwa mkono lakini wakili Charwe alisema yaliungwa mkono,”walisema.

Hata hivyo, majaji hao walisema baada ya kupitia mawasilisho ya mawakili wa pande mbili,  na kwa kuzingatia ushahidi wa shahidi wa 3,6,14,15 na 21, wanaona kulikuwa na ushahidi wa kutosha kuunga mkono maelezo ya warufani hao.

“Katika tukio lililotokea tarehe 25.12.2014 eneo la Majengo ambapo mmoja wa washambuliaji alikufa, simu ambayo ni kielelezo cha 16 ilipatikana na ilipochunguzwa, mawasiliano yake yalisaidia kukamatwa mrufani wa Pili”

Kulingana na ushahidi wa shahidi wa 21, mrufani huyo alikiri kushiriki matukio hayo ya ugaidi akiwa pamoja na kiongozi wao ambaye ni mshitakiwa wa kwanza na ni kutokana na kukiri kwake huko, ndio washirika wake hao nao walikamatwa.

“Ni mtizamo wetu kuwa ushahidi wa mazingira unawaunganisha warufani na makosa kwa kuegemea ushahidi wa simu. Tumeridhika kuwa hata bila uwepo wa maelezo ya mrufani wa tatu, kukiri kwake kwa mdomo kunamuunganisha.

“Katika mazingira haya, hatuoni sababu yoyote ya msingi katika hoja za warufani kuwa ushahidi wa baadhi ya mashahidi ulikuwa unajichanganya kutoka kwa mmoja kwenda kwa mwingine. Kwa hiyo hata sababu ya pili ya rufaa inatupwa”

Ni kwa msingi huo, majaji waliitupilia mbali rufaa hiyo kwa kutokuwa na mashiko.