Unguja. Wakati India ikiwa moja ya mataifa yaliyoendelea katika masula ya afya na teknolojia, kampuni kubwa kutoka nchini humo zimeonesha nia ya kuwekeza Zanzibar katika sekta za viwanda na tiba hususani katika ujenzi wa kituo maalumu cha kutoa matibabu ya kibingwa.
Hatua hiyo imefikiwa baada ya kampuni zaidi ya 20 kutoka nchini humo kufika kisiwani hapa na kuangalia maeneo yenye fursa za uwekezaji katika sekta mbalimbali wakiongozwa na balozi wa Tanzania nchini India, Anisa Kapufi Mbega.
Akizungumza katika jukwaa la biashara na uwekezaji baina ya Zanzibar na India Julai 19, 2025, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Kazi, Uchumi na Uwekezaji, Shariff Ali Shariff ametaja eneo lingine ambalo ujumbe huo umeonesha dhamira ya kuwekeza ni katika masuala ya viwanda na dawa za binadamu.
“Wakiwekeza kwenye eneo hili maana yake hakuna tena safari za kwenda India kupata matibabu, hatua hiyo itapunguza gharama za wagonjwa kusafirishwa, muda na kuongeza ujuzi wa watalamu wetu hapa nchini,” amesema Shariff.
Amesema India wanapenda vyakula vya viungo hivyo ni moja ya maeneo pia ambayo wanataka kuyatilia mkazo ikiwemo karafuu na viungo vingine.
“Ukiangalia idadi ya watu wa India ni wengi sana, baada ya China ni India kwa hiyo soko lipo hivyo kilichobaki ni sisi kujipanga vizuri katika soko la bidhaa za viungo,” amesema.
Shariff amesema kati ya wawekezaji hao wapo waliokuja kufanya utafiti wa viungo hivyo nalo ni eneo ambalo linaangaliwa kwa ukaribu ikizingatiwa India ni miongoni mwa mataifa yanayopenda viungo (spice).
Amesema licha ya Zanzibar kuwa kisiwa kinachozalisha viungo vingi lakini bado hakijawa na uwezo mkubwa wa kuitangaza kwa hiyo ujio wa wawekezaji kutoka India ni fursa itakayotumika kutangaza bidhaa hiyo.
Amesema kwa sasa Serikali imetenga maeneo maalumu kwa ajili ya kuzalisha bidhaa za ndani na za nje kwa kuleta mali ghafi.
“Sera za Serikali ni kukuza viwanda, kwa sasa bado hatupo vizuri lakini tunaelekea huko katika kuwekeza kwenye viwanda vyepesi, maeneo yapo tunataka wawekezaji waje mazingira yamewezeshwa,” amesema.
Mkurugenzi wa Taasisi ya Utafiti na Masoko ya nchini India (MARS), Rekha Sharma amesema wameongoza na kampuni takribani 25 za India kutoka sekta mbalimbali za utalii, viwanda, hoteli, huduma na masuala ya fya.
“Hii ni katika kutafuta fursa za uwekezaji, kuwekeza Zanzibar na Tanzania, kwa hiyo kuna programu saba ambazo zinatakribani Dola za Marekani milioni saba, wawekezaji tumepanga wakati huu kuja kuwekeza Zanzibar na kampuni zaidi zmeonyesha nia ya kuwekeza Zanzibar katika sekta ya dawa na elimu,” amesema.
Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Kukuza Uwekezaji Zanzibar (Zipa), Saleh Saad Mohamed amesema safari hiyo imeandaliwa na Zipa na taasisi binafsi ya Mars kwa kushirikiana na ubalozi wa Tanzania nchini humo ili waje kutambua fursa zilizopo Zanzibar.
“Huu ni mwendelezo wa kupokea wageni, india ni moja ya nchi zinazoendelea kuonesha nia ya uwekezaji katika nyanja mbalimbali.
“Maendeleo ya ushirikiano baina ya Serikali hizi na wadau itapelekea kuleta wawekezaji wengi hususani katika viwanda vya nguo na viwanda vya kuchakata mazao na wengine katika uwekezaji wa hoteli,” amesema.
Balozi wa Tanzaia nchini India Anisa Mbega amesema wamekuja na wawekezaji 20 wameonesha kuwekeza Zanzibar.
“Tupo kwa ajili ya kutafuta fursa ambazo zitatusaidia katika kuinua uchumi wetu, tunafahamu jitihada kubwa zinazofanywa na viongozi wetu wa kitaifa, katika kuboresha mazingira ya uwekezaji, kuvutia wawekezaji kuja kwenye mataifa haya mawili kuwekeza katika sekta mbalimbali na kuongeza kipato kwa wananchi wetu,” amesema.