Arusha. Jumuiya ya wataalamu zaidi ya 700 wa usimamizi wa rasilimali watu na utawala katika utumishi wa umma (TAPA-HR), wanatarajiwa kukutana jijini Arusha katika mkutano mkuu wa kwanza wa jumuiya hiyo.
Mkutano huo utakaoanza Julai 22 hadi 25,2025 katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha (AICC), utafunguliwa na Waziri Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, George Simbachawene.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Arusha leo, Mwenyekiti wa TAPA-HR, Grace Meshy,amesema mkutano huo unalenga kuwajengea uwezo zaidi wataalamu hao na kuongeza tija katika ufikiaji wa malengo makuu ya taasisi zao na ustawi wa wananchi kwa ujumla.
Amesema mkutano huo utawakutanisha wataalamu wa kada ya usimamizi wa rasilimaliwatu na utawala katika utumishi wa umma kutoka Tanzania bara na visiwani.
“Mkutano wetu utaongozwa na kaulimbiu isemayo,“Mwelekeo mpya wa nafasi ya wataalamu wa usimamizi wa rasilimaliwatu na utawala: kusukuma mabadiliko, kuendana na mageuzi ya teknolojia kwa ajili ya kuboresha huduma katika utumishi wa umma’’amesema
Mwenyekiti huyo ametumia nafasi hiyo kuwaomba waajiri wote katika Wizara, Tawala za Mikoa Mamlaka ya Serikali za Mitaa, wakala za Serikali, mashirika ya umma, vyuo vikuu na vyuo vikuu vishiriki kuwawezesha wataalamu wao kushiriki mkutano huo muhimu kwa tasnia hiyo.
Grace amesema kuwa Jumuiya hiyo iliundwa ili kutekeleza malengo saba ikiwemo kuhakikisha kunakuwa na fursa ya kubadilishana uzoefu katika masuala ya usimamizi wa rasilimaliwatu na utawala, kukuza ujuzi na weledi katika masuala ya usimamizi wa rasilimaliwatu na utawala.
Nyingine ni kuhifadhi na kusambaza taarifa za kitaaluma katika kada ya usimamizi wa rasilimaliwatu na utawala kwa njia ya machapisho, mikutano, ziara za mafunzo, makongamano ya kitaaluma, midahalo na kuweza kujiunga na mitandao ya kitaaluma ya kitaifa na kimataifa.
“Malengo mengine ni kuimarisha maadili ya kitaaluma katika masuala ya usimamizi wa rasilimaliwatu na utawala, kukuza ushirikiano wa kitaifa na kimataifa kupitia mashirika na taasisi zinazojishughulisha na ukuaji na usimamiaji wa rasilimali watu,”amesema.
Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo, Ally Ngowo amesema siku ya mwisho ya mkutano huo kutakuwa na bonanza kwa ajili ya michezo mbalimbali litakaloshirikisha wataalamu wote.
“Tutakuwa na michezo mbalimbali ikiwemo mpira wa miguu kwa wanaume,mpira wa pete kwa wanawake, kukimbia na michezo mingine mingi,”amesema makamu huyo.