TCU: Hatutayumba kusimamia ubora wa elimu ya juu

Unguja. Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) imesisitiza dhamira yake ya kusimamia elimu ya juu kwa ufanisi, ili kuhakikisha kuwa wahitimu wa vyuo vikuu nchini wanakuwa na viwango vya kimataifa na kukubalika duniani kote.

Mwenyekiti wa Tume hiyo, Dk Leonard Akwilapo ametoa kauli hiyo leo Julai 19, 2025 katika maonesho ya sita ya elimu ya juu yanayofanyika katika viwanja vya Mnazimmoja kisiwani Zanzibar na kuwashirikisha vyuo vikuu na taasisi za uwakala wa kupeleka wanafuzi nje ya nchi.

“TCU itakuwa tayari kushirikiana na taasisi zote za elimu ya juu katika azma ya kuimarisha eneo la elimu ya juu hususani kuimarisha suala zima la ubora, tutaendelea kusimamia kwa dhati elimu ya ubora ili wahitimu waendelee kuwa na viwango vya kimataifa na kukubalika popote watakapokwenda duniani, hii ni azma yetu haitateteleka hata siku moja,” amesema Dk Akwilapo.

Amesema katika maonesho hayo taasisi hizo zimepata wanafunzi wengi ambao wanaka kujiunga na eimu ya juu na kupatiwa miongozo na usauri kuhusu programu mbalimbali.

“Bila shaka mmepata wateja wengi ambao wamependa kujua aina mbalimbali za programu mnazotoa katika vyuo vyenu, hili ni jambo muhimu sana kwa mwanafunzi kufanya uamuzi sahihi kabla ya kuanza masomo,” amesema Dk Akwilapo


Amesema kwa kawaida mwanafuzi akishakosea mwanzoni katika kufanya uamuzi sahihi inakuwa vigumu kufanya marekebisho mbele ya safari ‘kwa hiyo tunashukuru Wizara ya Elimu kuandaa shughuli hii ambayo imewasaidia sana wanafunzi wetu.”

Mkurugenzi wa Uhusiano na wadau wa elimu ya ndani na nje ya nchi kutoka Global Education Link, Robert Kibona amesema kwa miaka sita sasa taasii hiyo inashiriki maonesho ya wiki ya elimu kuwaonyesha wanafunzi fursa kwenda kusoma nje ya nchi kupitia vyuo ambavyo wanashirikiana navyo katika kozi mbalimbali kwa manufaa ya wanafunzi wenyewe lakini na kwa serikali na taifa.

“Wanafunzi wasipate shaka kuhusu usalama na ubora wa elimu wanayokwenda kuipata nje ya nchi sio tu kwamba tunawasaidia kupata udahili pekee lakini wanapata kwenye vyuo vinavyotambulika kimataifa na programu ambazo zinatambulika kimataifa,” amesema.

Amesema wakishadahiliwa wanawasindikiza na kupata mahitaji ya mwanzo na hawaachwi bali wanafuatilia mwenendo wao kitaaluma na kuhakikisha wanahudhuria masomo kwa mujibu wa ratiba.

“Tumeshaunganisha mfumo wa wanafunzi wanaodahiliwa na mfumo wa Global Education Link kwa hiyo tunawafanyia monitoring mpaka wanapohitimu kwa hiyo ikitokea mwanafunzi hajahudhuria darasani hata kama ni siku moja tunajua, hata wakipata changamoto wakiwa chuoni tunazitatua au kama zinahitaji kuwasiianana wazazi tunawasiliaan nao,” amesema.

Tangu ianze kudahili wanafunzi kwenda kusoma nje ya nchi mwaka 2007, wanapeleka nje ya nchi wastani wanafunzi 500 kila mwaka.

“Tumefanikiwa kwa kiasi kikubwa wanafunzi wanaopelekwa nje kusoma hawajutii bali wanaona manufaa yake,” amesema.

Amesema baada ya maonyesho hayo Global Education Link wamendaa maonesho mengine ambayo yatafanyika katika mikoa ya Dar es Salaam, Arusha na Kahama ikiwa lengo ni lile la kuwaonyesha wanafunzi fursa na kujua namna ya kufikia ambapo tayari kuna vyuo 20 ambavyo ni washirika kutoka nje ya nchi vitashiriki katika maonyesho hayo zikiwemo kozi za akili mnemba (AI).

Naye Meneja wa tawi la Zanzibar wa Global Education Link, Zulfiya Lablulal amesema kwa Wazanzibari wana fursa ufadhili hadi asilimia 100 “kwa hiyo wanafunzi wanakaribishwa kwa ajili ya kujipatia fura hiyo.”

Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali, Khalid Massoud Wazir amesema maonesho hayo yamekuwa na manufaa makubwa kwa wananchi na wanafunzi kupata fursa za masomo ndani na je ya nchi.

Amesema wakati maonyesho hayo yanaanza mwaka 2020, yalianza na washiriki 13, lakini kwa mwaka huu tayari wamefikia washiriki 80 hivyo imani yao wataendelea kuyaboresha na kufikia malengo makuu ya kuhakikisha elimu inapatikana kwa njia nyepesi.

“Huko tunakwenda tutapata tija kubwa, lengo kubwa ni kuwapati wanafunzi hususani wapya wanaotaka kujiunga na elimu ya kati na juu miongozo na taratibu ya kuijunga na vyuo hivyo,” amesema.