Dar es Salaam. Mvutano wa zaidi ya dakika 63 umeibuka kati ya wananchi wa Mabibo na Posta Saccos wakati Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila alipofika kutatua mgogoro wa ardhi katika aneo la Uwanja wa Sahara.
Uwanja huo ambao mpaka sasa haujaendelezwa na unatumika kwa ajili ya michezo mbalimbali, kwa mujibu wa sheria umiliki uko chini ya Shirika la Akiba na Mikopo la Posta na Simu (Posta ana Simu Saccos), jambo ambalo wananchi wanalipinga.
Hiyo ni baada ya wananchi kudai kuwa eneo hilo liliuzwa kinyume cha sheria kwani hakukuwa na muhtasari wa mauziano ambao ulijumuisha makubaliano ya waliokuwa wanachama wa Akilimali Mabibo Cooperative Society.
Akizungumza katika utatuzi wa mgogoro huo, Ahmed Aoni kutoka Posta na Simu Saccos amesema kwa mujibu wa sheria, wao ndiyo wamiliki halali wa uwanja huo kwani waliununua mwaka 1994 kutoka ushirika wa Akilimali Mabibo Cooperative Society ambao walikuwa wakimiliki wake.
Amesema wakati wakijikusanya ili wauendeleze mwaka 2001 uwanja huo ulifutiwa umiliki na Rais wa wakati huo, jambo lililofanya wao kwenda kufungua kesi mahakamani na mwaka 2006 walirudishiwa umiliki wa uwanja huo.
Baadaye mwaka 2007, walipeleka vifaa vya zaidi ya Sh100 milioni ikiwemo kibali cha kuweka uzio lakini kwa sababu eneo hilo lilikuwa likitambuliwa kama eneo la wananchi, walikutana na ugumu, jambo lililowafanya waanze kuwaelewesha wananchi kuwa eneo hilo ni lao.
“Eneo hili likiwa na ukubwa wa mita za mraba 19,410 ni la kwetu, tunamiliki kihalali, tuna hati, tuna hukumu ya Mahakama Kuu. Tunaamini kuwa sisi tunamiliki eneo hili, waliopo jirani ni majirani zetu, mpango wetu si kuwavunjia waliojenga, tuone tutafanya nini,” amesema.
Amesema kuwapo kwa mgogoro baina yao na wananchi umekuwa ukiwafanya washindwe kupata wawekezaji kwani kila aliyefika serikali za mitaa kwa ajili ya kuwekeza, aliambiwa kuna mgogoro.
Akipinga hoja hizo, Mjumbe wa Akilimali Mabibo Cooperative Society, Ngwisa Mwakyanjala amesema eneo hilo lilitengwa na wananchi kwa ajili ya eneo la watoto kucheza na watu kufanya mazoezi.
Baada ya eneo hilo kutengwa lilitolewa wazo la kuanzishwa kwa ushirika ambao ulimilikishwa hati ya eneo hilo huku likiendelea kutumika katika shughuli za michezo, kijamii na Serikali.
Hata hivyo, mwaka 2002 walishangaa kuona watu wameweka banda na walipohojiwa walisema wanataka kuanza kufanya ujenzi, jambo ambalo liliwashtua na kuwafanya waende kutoa taarifa kuwa eneo lao limeuzwa kupitia chama cha ushirika.
Amesema walipofika waliona ushirika bado upo hai na walihoji utaratibu wa kuuza mali za ushirika ukoje, ndipo walijibiwa kuwa ni lazima ofisa ushirika ahusishwe ili kujua kwa nini mali inauzwa na kama ni ushirika umekufa, kwa nini umekufa, wakaguzi wapite na wakijiridhisha na kujua madeni yaliyopo.
“Baada ya hapo, tunatangaza utaratibu wa mnada ndipo mnunuzi ndiyo anapatikana, tukawaambia wamenunua posta na akiba, akasema mauziano hayo ni batili kisheria walitakiwa kuwa na muhtasari wa wanaushirika,” amesema.
Amesema wananchi wanatamani eneo hilo litumike kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha afya ili kusaidika katika kupata huduma muhimu kwa urahisi.
Mkuu wa Idara ya Mipango Miji na Ardhi kutoka Ofisi ya Mkoa wa Dar es Salaam, Emmanuel Richard amesema kwa mujibu wa kumbukumbu, eneo hilo awali lilikuwa kwa ajili ya kuchezea watoto na shughuli za kijamii.
Baadaye, eneo hilo lilipimwa na kupewa namba 794 kitalu B Mabibo mwaka 1985 likiwa na ukubwa wa hekta 1.91 na baadaye lilimilikishwa kwa Akilimali Mabibo Cooperative Society na walipewa hati Januari mosi, 1985.
Amesema kwa mujibu wa kumbukumbu zilizopo mwenyekiti wa ushirika huo aliiuzia Posta eneo hilo ambapo mpaka sasa nyaraka zinaonyesha wao ndiyo wamiliki halali.
Kutokana na jambo hilo kutooneka kuwaridhisha wakazi wa Mabibo, Chalamila ameomba wiki moja ya kufanyia kazi suala hilo kupitia timu maalumu aliyoiunda.
Timu hiyo inajumuisha wanachama wa ushirika wa vyama hivyo viwili na viongozi wa idara mbalimbali ndani ya ofisi yake ili wapitie nyaraka zote muhimu kuhakikisha uamuzi unaotolewa unakuwa wa haki.
“Mnipe wiki moja, nitarudi tena hapa baada ya kupitia nyaraka zote muhimu,” amesema Chalamila.