UONGOZI wa maafande wa Tanzania Prisons, unafikiria kumrejesha aliyekuwa kipa wa kikosi hicho, Benedict Haule, baada ya kutokuwa na nafasi ya kucheza mara kwa mara katika timu ya Singida Black Stars kutokana na ushindani mkubwa uliokuwapo.
Haule aliyejiunga na Singida Black Stars Julai Mosi 2024, akitokea Tanzania Prisons aliyoichezea kwa mkopo kutokea Azam FC, anahitajika na timu hiyo kwa ajili ya kuongeza nguvu msimu ujao, huku akiwa tayari kurudi tena kukitumikia upya kikosi hicho cha maafande.
Hata hivyo, chanzo kutoka ndani ya kikosi hicho, kimeliambia Mwanaspoti kwamba, Tanzania Prisons inamuhitaji kipa huyo kwa mkopo wa msimu mzima wa 2025-26 na sio kumnunua moja kwa moja, jambo wanaloamini linaweza kurahishisha dili hilo kukamilika mapema.
“Makubaliano yanayoendelea ni ya kumpata kwa mkopo wa msimu mmoja na wala sio kumnunua moja kwa moja, tunachohitaji ni kuona tunafanya maboresho makubwa na yenye kuzingatia mahitaji muhimu ya kikosi,” alisema mmoja wa viongozi wa Prisons.
Haule ameshindwa kupenya katika kikosi cha kwanza kutokana na ubora wa Metacha Mnata na Mnigeria Amas Obasogie, ambaye tangu ajiunge na timu hiyo katika dirisha dogo la Januari 2025, akitokea Fasil Kenema FC ya Ethiopia amekuwa chaguo la kwanza.
Tanzania Prisons ilimaliza katika nafasi ya 13 kwa pointi 31 katika Ligi Kuu Bara msimu wa 2024-25 na kukwepa janga la kushuka daraja, baada ya kucheza mechi za ‘play-offs’ ikiichapa Fountain Gate iliyomaliza ya 14 kwa pointi 29 kwa jumla mabao 4-2.
Kutokana na kumaliza nafasi hiyo na kuepuka janga la kushuka daraja, kumewafanya mabosi wa Tanzania Prisons kuanza harakati hizo za usajili mapema, kwa lengo la kupata wachezaji bora na wazoefu watakaokipigania kikosi hicho cha maafande msimu ujao.