KIPA wa Dodoma Jiji, Mkongomani Alain Ngeleka huenda asiwe tena sehemu ya kikosi cha timu hiyo kwa msimu ujao, baada ya ujio wa Castor Mhagama kutoka KenGold, huku ikielezwa kuwa ishu ya nidhamu inaweza pia kuchangia kuondolewa kikosini.
Hivi karibuni, nyota huyo alisimamishwa katika timu hiyo kwa tuhuma za utovu wa nidhamu, ingawa taarifa ambazo Mwanaspoti imezipata kutoka ndani ya uongozi wa kikosi hicho zinaeleza kwa sasa asilimia za kubaki kipa huyo msimu ujao ni ndogo.
“Ngeleka ana mkataba wa mwaka mmoja uliobaki lakini uongozi unapanga kumuuza au ikishindikana wamtoe hata kwa mkopo msimu ujao, taratibu hizo zimeanza na ndio maana tumeanza kutafuta kipa mwingine mbadala wake,” kilisema chanzo chetu.
Ofisa Habari na Mawasiliano wa Dodoma Jiji, Moses Mpunga alipotafutwa na Mwanaspoti kuzungumzia suala hilo, alisema ni mapema kuweka wazi masuala yote yanayohusu usajili, hivyo apewe muda hadi taratibu zitakapokamilika watazitolea taarifa.
Ngeleka aliyemaliza na ‘clean sheet’ saba za Ligi Kuu Bara msimu wa 2024-25, inaelezwa hana uhusiano mzuri na mabosi wa timu hiyo akituhumiwa kwa utovu wa nidhamu uliosababisha kusimamishwa, hivyo nafasi yake ya kubakia ni ndogo msimu ujao.
Kipa huyo aliyejiunga na Dodoma Jiji msimu wa 2024-2025 akitokea Kagera Sugar, anakumbukwa zaidi msimu wa 2022-23 wakati akiwa na kikosi cha Tabora United FC zamani Kitayosce, ambapo aliweka rekodi nzuri ya kufunga bao katika Ligi ya Championship.
Ngeleka alifunga bao la kufutia machozi kwa upande wa Tabora United katika mechi kali na ya kusisimua iliyopigwa kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo, Mbweni jijini Dar, ambapo timu hiyo ilichapwa mabao 3-1 dhidi ya JKT Tanzania, Desemba 3, 2022.
Nyota huyo alijiunga na Tabora United wakati inashiriki Ligi ya Championship msimu wa 2022-23, akitokea klabu ya Lumwana Radiant ya Zambia, akizichezea pia Nkana na Buildcon za Zambia, Sanga Balende, Groupe Bazano na Tshinkunku FC za kwao DR Congo.