NI rasmi sasa Che Malone Fondoh hatakuwa sehemu ya kikosi cha Simba msimu ujao, hii ni baada uongozi wa timu hiyo kukamilisha biashara ya kumuuza kwa timu iliyotuma ofa ya kumuhitaji mwishoni mwa msimu uliomalizika.
Che Malone, alitua Msimbazi misimu miwili iliyopita akitokea Coton Sport ya Cameroon na kutengeneza ukuta mgumu akianza kucheza sambamba na Henock Inonga msimu wa kwanza, kisha Abdulrazack Hamza na Chamou Karaboue.
Beki huyo wa kati licha ya kutokuwa na msimu mzuri kama ilivyokuwa msimu wake wa kwanza alipojiunga na timu hiyo kutokana na kusumbuliwa na majeraha, aliingia kwenye rada za USM Alger ambayo imemaliza msimu wa Algeria ikiwa nafasi ya nane kwenye msimamo.
Chanzo kutoka ndani ya Simba kimesema mchakato walioanza nao mwezi mmoja nyuma kwa kufanya mazungumzo na USM Alger umekamilika na kufanikisha kufanya biashara na timu hiyo.
Hata hivyo, Mwanaspoti linafahamu kuwa uongozi wa Simba na benchi la ufundi la timu hiyo hawakuwa na mpango wa kuendelea na beki huyo kwa ajili ya msimu ujao ndio maana imekuwa rahisi kwao kufanya biashara.
“Ni kweli tumemalizana na timu hiyo na mchezaji ataitumikia baada ya biashara kufanyika, Che Malone alibakiza mkataba wa mwaka mmoja ambao timu hiyo ndio imeamua kuulipia, hivyo sasa sio sehemu ya kikosi chetu,” alisema mtoa taarifa huyo na kuongeza.
“Nafikiri mwanzo uliniuliza nilishindwa kulithibitisha hilo kwa sababu nilikuwa sina uhakika nalo, lakini sasa ni wazi kuwa biashara imeshafanyika.”
Mtoa taarifa huyo ambaye hakutaka jina lake litajwe gazetini, alisema ofa ya mchezaji yeyote ambaye wanammiliki ikienda mezani kwao wataipokea na kuiangalia kama ina maslahi mapana kwao na kwa mchezaji hawana sababu ya kuiacha iende, watafanya biashara kwani hawana sababu ya kuendelea kuwang’ang’ania wachezaji wao.
Usajili wa Che Malone kwenda USM Alger, umekuja baada ya klabu hiyo kuachana na beki wake wa kati, Kevin Mondeko ambaye mkataba wake umemalizika.
Ukiachana na Che Malone, Mwanaspoti linafahamu kuwa Simba pia ipo kwenye hatua nzuri ya kumalizana na RS Berkane kwa ajili ya kumuuza mshambuliaji wake Steven Mukwala ambaye amemaliza msimu vizuri akifunga mabao 13 kwenye Ligi Kuu Bara.
Che Malone anakuwa mchezaji wa saba kuondoka Simba dirisha hili baada ya Hussein Kazi, Fabrice Ngoma, Valentin Nouma, Augustine Okejepha, Debora Fernandes na Omary Omary aliyepelekwa Mashujaa kwa mkopo.